
- Zaidi ya wageni 500 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na kwingineko duniani wamehudhuria Kongamano la Kimataifa la Dini mkoani Arusha na kuondoa hofu yoyote iliyokuwepo kuhusu hali ya usalama nchini, huku wakikemea kampeni chafu zinazoendeshwa mtandaoni kwa lengo la kuvuruga sekta ya utalii nchini Tanzania.
Washiriki hao, wengi wao wakifurahia amani na utulivu walioushuhudia tangu kuwasili kwao siku tano zilizopita, walitoa wito kwa Watanzania kupambana na vitisho na "hashtagi" za uzushi zinazolenga kuzuia wageni kuingia nchini.
Akizungumza kwa masikitiko, Bi. Joela Athumani, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alieleza jinsi yeye na wenzake walivyokuwa na wasiwasi mkubwa kabla ya safari yao kutokana na taarifa za kupotosha zinazozagaa mitandaoni.
"Wakati tunakuja Tanzania tulisikia vitu vingi, tukaangalia kwenye runinga na tukaona habari za uwepo wa machafuko, tukawa na wasiwasi wa Kongamano letu kiasi cha kuanza kufikiria kuahirisha," alisema Bi. Joela.
Hata hivyo, baada ya kufika nchini, alishuhudia hali tofauti kabisa: "Tunashukuru Mungu tumefika na tumekuta amani ya kutosha. Mungu ni mwema sana kwasababu amewezesha amani Tanzania, tunamshukuru sana Mungu."
Bi. Joela amewataka Watanzania kuishikilia kwa nguvu baraka ya amani waliyopewa, huku akiwahakikishia wale wote waliopanga kuja nchini kutokuwa na wasiwasi wowote wa kiusalama kwani hali ni shwari na shughuli zinaendelea kama kawaida.
Akitoa ushuhuda wa athari za moja kwa moja za uvunjifu wa amani, Bw. Ogi Kabongo, mkazi wa Kinshasa, DRC, alitumia uzoefu wa nchi yake kuonya Watanzania.
"Ukosefu wa amani unadhoofisha na kuua kabisa ustawi na maendeleo ya wananchi," alieleza Bw. Kabongo, huku akiwataka Watanzania kudumisha amani ya nchi yao kwa gharama yoyote ile.
Naye Bw. Fransis Owusu, raia wa Senegal na Rais wa Shirika la Full Gospel Business Men's Fellowship International, alisisitiza umuhimu wa amani katika sekta ya kiuchumi.
"Amani hiyo mara zote imekuwa msingi muhimu wa maendeleo na kiwezeshi kikubwa cha mafanikio katika shughuli za kiuchumi," alisema Bw. Owusu, akiiomba jamii kuendelea kuiombea amani ya Tanzania.
Mkutano huo wa kimataifa wa siku mbili, uliokusanya wajumbe zaidi ya 500 kutoka mataifa mbalimbali, ulilenga kujadili mchango wa dini katika uchumi na maendeleo. Matukio ya aina hii yanathibitisha kuwa, licha ya upotoshaji mtandaoni, Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani kinachovutia makongamano na watalii wa kimataifa.