` UHARIBIFU WA OFISI 756 UNAVYOUUA UCHUMI WA MTANZANIA

UHARIBIFU WA OFISI 756 UNAVYOUUA UCHUMI WA MTANZANIA



Kauli ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, iliyotaja takwimu za kutisha za uharibifu wa mali wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025,umefungua mjadala mzito kuhusu athari za vitendo hivi katika uchumi wa nchi. Uchambuzi unaonesha kwamba uharibifu huo si tu hasara ya mali, bali ni adhabu ya moja kwa moja kwa kipato, huduma za jamii, na maisha ya kila Mtanzania.

Takwimu za uharibifu wa Ofisi za Serikali 756 na Vituo vya Polisi 159 zina maana moja kubwa kwamba kiasi kikubwa cha fedha za umma, ambacho kilitakiwa kuelekezwa kwenye ujenzi wa shule mpya, zahanati, au miundombinu ya maji, sasa lazima kitumike kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.

Kama Waziri Mkuu alivyosema, fedha zinazotekeleza miradi ni za Watanzania, uharibifu huu umepunguza mtaji wa taifa na una maana kwamba mipango mingi ya maendeleo itakwama au itachelewa, huku gharama za kujenga upya zikipanda kutokana na mfumuko wa bei.

Uharibifu mkubwa wa mali za watu binafsi umeathiri mfumo mzima wa kiuchumi, hasa kwa wale wanaojitegemea. Uharibifu wa pikipiki 2,268 umewaondoa ghafla maelfu ya vijana kwenye biashara ya bodaboda, ambayo ni chombo chao cha kwanza cha riziki. 

Vilevile, Magari 1,642 ya watu binafsi, ambayo mengi yanatumika kama magari ya kukodi au usafirishaji, yameathirika, na kusimamisha biashara hizo kabisa.

Wakati huo huo, uharibifu wa vituo 27 vya Mwendokasi na mabasi 6 unavuruga mfumo wa usafiri wa umma, ambao ni muhimu kwa tija ya wafanyakazi.

Waziri Mkuu alisema: "Maisha ya Mtanzania mmojammoja ni ya kutoka eneo moja aende eneo jingine; hawa watu wasipotoka unataka wale nini?"

Uchambuzi huu unathibitisha kuwa uharibifu huo ulikuwa na lengo la wazi la kuwapiga Watanzania masikini na wa kipato cha kati, ambao hawawezi kujilimbikizia mali na wanategemea usafiri wa kila siku hivyo kuchochea hasira dhidi ya serikali.

Uharibifu wa magari ya Serikali 976, ikiwemo ambulansi, una athari mbaya kwa huduma za dharura. Katika hali ya majanga au uhitaji wa haraka wa matibabu, kupungua kwa idadi ya ambulansi kunahatarisha moja kwa moja maisha ya Watanzania. Vilevile, kuchomwa kwa vituo vya Polisi kunadhoofisha ulinzi na usalama wa raia, na hivyo kupunguza imani ya wawekezaji.

Kama Dkt. Mwigulu alivyoelezea, vitendo vya Oktoba 29 vilikuwa hujuma ya kiuchumi iliyopangwa. Kwa kulenga miundombinu muhimu ya usafiri, nishati, na usalama, waharibifu walitaka kusimamisha mzunguko wa pesa na riziki za Watanzania. 
Hivyo, gharama ya urejeshaji wa hasara hii itabebwa na mabega ya kila Mtanzania kupitia kodi, huku miradi ya maendeleo ikisubiri.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464