` TISEZA, TCB WAHIMIZA WATANZANIA WAISHIO NJE KUWEKEZA NYUMBANI

TISEZA, TCB WAHIMIZA WATANZANIA WAISHIO NJE KUWEKEZA NYUMBANI

 




TISEZA, TCB WAHIMIZA WATANZANIA WAISHIO NJE KUWEKEZA NYUMBANI

Na Mwandishi Wetu
Toronto, Canada

Katika jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Watanzania wanaoishi nje ya nchi, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Huru ya Uzalishaji Tanzania (TISEZA), kwa kushirikiana na Benki ya TCB na Ubalozi wa Tanzania nchini Canada, imefanya mikutano ya uwekezaji ya ngazi ya juu katika miji ya Toronto na Calgary.

Mikutano hiyo iliwakutanisha Watanzania waishio Canada, ambapo walipatiwa taarifa za kina kuhusu fursa za uwekezaji nchini Tanzania pamoja na huduma za kifedha zinazotolewa na Benki ya TCB kwa ajili ya wawekezaji binafsi na wa taasisi.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Gilead Teri, alisema serikali imejipanga kuhakikisha diaspora inashiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa taifa kupitia uwekezaji endelevu.

“Watanzania wanaoishi nje ni sehemu muhimu ya safari ya maendeleo ya nchi yetu. Tunataka wawe sehemu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuwekeza kwenye miradi inayochochea ajira na ukuaji wa taifa,” alisema Bw. Teri.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Canada, Mhe. Joseph Sokoine, aliipongeza TISEZA na TCB kwa kuandaa majadiliano hayo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mawasiliano ya karibu na diaspora.

“Mazingira ya uwekezaji Tanzania ni rafiki zaidi kuliko wakati wowote. Ni wakati sasa kwa Watanzania wanaoishi nje kutumia fursa hizi ili kuwekeza nyumbani, wakijijengea kipato huku wakichangia maendeleo ya taifa,” alisema Mhe. Sokoine.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Rejareja na Biashara Ndogo na za Kati wa TCB, Bi. Lilian Mtali, aliwasilisha huduma maalum zinazotolewa kwa Watanzania waishio nje ya nchi, zikiwemo akaunti za uwekezaji, mikopo na huduma za kidijitali zinazorahisisha miamala kutoka nje ya nchi.

“TCB imejipanga kuhakikisha Watanzania waishio nje wanapata huduma salama, nafuu na zenye ubunifu zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa,” alisema Bi. Mtali.

Mikutano hiyo ilipokelewa kwa hamasa kubwa na Watanzania waishio Canada, ambapo washiriki wengi walionesha nia ya kuwekeza katika sekta za ardhi na nyumba, kilimo, utalii na viwanda.

Juhudi hizi zinatajwa kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa sera ya diplomasia ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, zikilenga kutumia ipasavyo nguvu ya Watanzania wanaoishi nje kama washirika wa kimkakati katika kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464