
Wananchi na wadau mbalimbali wamelaani vikali vurugu zilizotokea hivi karibuni, wakisisitiza kuwa matukio hayo hayakuwa maandamano bali vitendo vya kihalifu vilivyochochewa na mihemuko ya mitandao ya kijamii.
Wamehimiza vijana kurudi kwenye misingi ya malezi na maadili bora, huku wakikataa ndoto za kutaka utajiri wa haraka bila kufanya kazi.
Bw. Juma Kasimu Kambangwa, mfanyabiashara wa Soko la Mvuti, alieleza utofauti kati ya maandamano halali na fujo iliyotokea: "Kwa kweli kwa muda wa wiki mzima hatuna biashara... hatujui kama yale yalikuwa maandamano au fujo kwani maandamano tunajua kuwa unakuwa na ujumbe, lakini kilichotokea ni kuharibiwa kwa mali za watu na miundombinu. Hatupendezewi na hali hiyo."
Alielekeza lawama kwa mtindo wa maisha unaoenezwa na mitandao ya kijamii, akisema vijana wanakosa uelewa wa hali halisi: "Vijana wamekuwa na mihemuko ya mitandao ya kijamii wanavyoona katika nchi nyingine na wao wanatamani wawe kama wao. Wao hawaangalii, wao wanataka leo wazaliwe kesho wawe matajiri." Bw. Kambangwa aliwaasa kufuata taratibu za kisheria na nchi na kuangalia athari kwa jamii kama zile zilizotokea.

Naye Bw. Hussein Thomas Mawanja alieleza kwa mshangao hali ya sasa, akisisitiza kuwa maisha halisi yanahitaji uvumilivu na kujituma: "Vijana wengi wa sasa hivi maisha hawayajui, maisha wanayaona kama maisha lakini maisha haya ni magumu ya kufuata mambo ya vishawishi vya ajabu." Alikumbusha Watanzania bahati ya amani waliyonayo, akisema: "Nimeenda Burundi na Rwanda, hali mbaya miaka ya 1990. Nchi iliyobaki Tanzania asikwambie mtu kwingine shida."
Kwa pamoja, wadau hawa wanatoa wito wa kitaifa kwa vijana kuacha tabia ya kuwa wahalifu na kutambua kuwa amani ya Tanzania si urithi wa kurithi bali inahitaji kulindwa kwa nidhamu na kufuata misingi ya maadili yaliyotukuka.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464