Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs),linalofanyika bure, ili kujua hali zao za afya na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dk. Luzila amesema, zoezi hilo litafanyika kuanzia leo Novemba 11 hadi 15,kwenye Viwanja vya Zimamoto, vilivyopo jirani na Soko la Nguzonane.
Amesema, Tanzania huadhimisha Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza duniani kila wiki ya pili ya mwezi Novemba, na kwa mwaka huu maadhimisho yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Chukua hatua kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.”
“Natoa rai kwa wananchi wote wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili wapate vipimo na elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Dk. Luzila.
Aidha, amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) za Septemba 2025, kwamba vifo milioni 43 ambavyo hutokea duniani vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Ametaja magonjwa ambayo yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani ikiwamo na Tanzania, kuwa ni magonjwa ya moyo, kisukari, figo, kansa, mapafu, shinikizo la damu,kiharusi na sekoseli.
Amesema, katika zoezi hilo la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza, kwamba wanatarajia kuwapata watu zaidi ya 500 kwa siku zote Tano
Baadhi ya wananchi ambao wamejitokeza kupata huduma hizo akiwamo Mpera Kibina, wameshukuru na kwamba wameweza kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akizungumza na waandishi wa habari.
Wananchi wa Shinyanga wakiwa wamejitokeza kupima Magonjwa yasiyoambukiza katika Viwanja vya Zimamoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



























