Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ya Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Dk.Charles Mlonganile akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto njiti yaliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali hiyo Novemba 17,2025
Sumai Salum-Kishapu
Hospitali ya Wilaya ya Kishapu Dr.Jakaya Mrisho Kikwete imeungana na jamii kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani, inayofanyika Novemba 17 kila mwaka, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu changamoto wanazokutana nazo watoto wanaozaliwa kabla ya muda na umuhimu wa kuwapa huduma stahiki.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Novemba 17,2025 hospitalini hapo Mganga Mfawidhi Dk.Charles Mlonganile amesema Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo “Wape Watoto Njiti Mwanzo Imara kwa Maisha Yenye Tumaini”, ikisisitiza malezi, uangalizi na huduma za kitaalamu kwa watoto hao.
Mlonganile amewahakikishia wanawake wote wanaojifungua watoto njiti kuwa huduma za kuwahudumia na kuwalea watoto hao zipo, zinafanyika kwa umakini mkubwa na zinaendelea kuimarishwa ili kuokoa maisha ya mama na mtoto. Amesema jitihada hizo zimekuwa zikisaidia kuongeza kiwango cha usalama na ustawi wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.
Akisoma taarifa ya Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Muuguzi kiongozi wodi ya watoto wachanga, Benjamin Bahati amesema huduma kwa watoto njiti zimeimarika tangu kukamilika kwa jengo la Wodi ya Watoto Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (NNU).
"Watoto wengi wanaozaliwa njiti sasa hupata huduma za dharura, uangalizi wa karibu, tiba, na ushauri wa wataalamu, kati ya Januari na Oktoba 2025, Watoto njiti 76 wamehudumiwa, huku baadhi yao wakihamishiwa vituo vya juu zaidi kwa matibabu ya kitabibu kulingana na hali zao" ameongeza
Aidha, baadhi ya wananchi walioshiriki maadhimisho hayo wakiwemo wanawake na wanaume wenye watoto njiti wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na wauguzi, wakisema kuwa juhudi zao zimekuwa mkombozi mkubwa kwa familia nyingi. Wameeleza kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma za watoto njiti na namna ya kuwalea kwa uangalifu.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kutoa shukrani na ushuhuda wao ni pamoja na Lucy Nkandi (Mhunze), Getrude Masenga Mwalata na Masele Joseph Luhende (Mwaweja) ambao wamesema wana imani kubwa na huduma zinazotolewa na wahudumu wa afya.
Hospitali imeendelea kutoa elimu kwa akina mama kuhusu njia sahihi za kuwalea watoto njiti ikiwemo njia ya Kangaroo Mother Care inayosaidia mtoto kupata joto na kuimarika kwa haraka.
Vilevile, takwimu zinaonyesha kupungua kwa vifo kutokana na huduma bora, ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano kati ya wahudumu wa afya na familia.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa kukata na kula keki ya pamoja na kugawa zawadi kwa kina mama wenye watoto njiti walioko wodini na nje ya wodi kutokana na michango binafsi ya watumishi wa Hospitali hiyo.