Na Mwandishi wetu- Manyara
Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua thabiti za kuimarisha mifumo ya usimamizi wa utendaji na uwajibikaji ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo halisi kwa wananchi.
Katika muendelezo wa juhudi hizo, viongozi na wataalam kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa wamekutana leo tarehe 25 Novemba, 2025 Mkoani Manyara katika kikao kazi maalum kilichojumuisha Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Tabora, Kilimanjaro na Dodoma kwa ajili ya kujadili na kuimarisha utekelezaji wa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini.
Akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonaz, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bi. Maryam Ahmed Muhaji amewashukuru washiriki kwa kujitokeza katika kikao kazi ambacho ni sehemu ya mafunzo, maagizo ya Serikali ya kuunganisha nguvu na kutumia mbinu za pamoja katika Kufuatilia na Kupima Utendaji kazi wa sekta za umma kwa ufanisi.
Aidha, ameeleza kuwa licha ya serikali kuwa na miongozo kadhaa ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa miaka ya nyuma, tathmini imeonesha kuna changamoto za kukosekana kwa uratibu na matumizi ya mifumo isiyounganishwa na kutegemea ufuatiliaji wa mchakato badala ya matokeo, pamoja na upungufu wa kufanya tathmini za mara kwa mara. Hali ambayo imeathiri upatikanaji wa taarifa sahihi kwa maamuzi ya kisera.
"Kutokana na changamoto hizo, Serikali imeandaa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini ambao unalenga kusanifisha mifumo, kuimarisha uwajibikaji, na kuhakikisha kwamba takwimu zinazokusanywa zinatumika kuongoza maamuzi, kupanga vipaumbele na kuboresha utekelezaji wa miradi Kitaifa", amesema Bi. Muhaji.
Pamoja na hayo amewakumbusha viongozi na wataalam majukumu yao kuhakikisha mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini unatekelezwa ipasavyo.
Hata hivyo amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuimarisha vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuviwezesha vitengo kuwa na rasilimali watu na fedha, huku Maafisa Mipango wakisisitizwa kuoanisha mipango na viashiria vinavyopimika tangu hatua za awali za miradi inayotekelezwa katika Halmashauri zao.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, anayeshughulikia sehemu ya Sekretarieti za Mikoa na Mamkaka za Serikali za Mitaa, Bw. John Bosco Quman alieleza umuhimu wa kikao hicho kwa viongozi hao ambao ni muhimili wa utekezaji wa shughuli za Serikali kuwa na muunganiko mzuri, ili kuhakikisha miradi na shughuli zote za Serikali zinatekelezwa kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha.




