` BIASHARA ZAENDELEA KAMA KAWAIDA SOKO KUU SHINYANGA

BIASHARA ZAENDELEA KAMA KAWAIDA SOKO KUU SHINYANGA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

WAFANYABIASHARA katika Soko Kuu la Mjini Shinyanga wameendelea na biashara zao kama kawaida,huku wakilalamikia baadhi ya bidhaa kuadimika.
Wamebainisha hayo leo Novemba 5,2025 wakati wakizungumza na vyombo vya habari vilivyotembelea sokoni hapo kuona hali ikoje ya kibiashara mara baada ya serikali kutangaza hali irejee kama kawaida kufuatia vurugu zilizojitokea kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Mmoja wa wafanyabiashara hao akiwamo Ayoub Amosi, amesema wanaishukuru Serikali kwa kurudisha hali ya amani, na sasa wanafanya biashara zao kwa amani na utulivu bila ya hofu yoyote,lakini baadhi ya bidhaa ambazo huzitegemea kutoka mikoa mingine zimeadimika.
“tunaishukuru serikali kwa kurejesha hali ya amani hapa nchini,sasa hivi wateja wanakuja kwa wingi tofauti na kipindi cha vurugu wakati wa Uchaguzi hali ilikuwa mbaya hakuna biashara kabisa,”amesema Amosi.

Mfanyabiashara mwingine Monica Charles,ambaye anauza Samaki wa kukaanga,amesema kufungwa Soko kabla ya wakati, walikuwa wakipata shida kumaliza bidhaa zao na hata kusababisha Samaki kuharibika na kuingia harasa.
Makamu Mwenyekiti wa Soko hilo Wiliam Nyaingi, ameiomba serikali kuendelea kuimarisha ulinzi na amani ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi bila usumbufu.

Nao baadhi ya wateja akiwamo Ashura Khamisi,amesema wanaishukuru Serikali kwa kurejesha hali ya amani na sasa wanafika sokoni bila hofu yoyote na kupata mahitaji muhimu.
Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amesema hali ya usalama mkoani humo, imeimarika na shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464