` KATAMBI ALIVYOTANGAZWA KUIBUKA MSHINDI UBUNGE JIMBO LA SHINYANGA MJINI,ASHINDA KWA KURA 131,126

KATAMBI ALIVYOTANGAZWA KUIBUKA MSHINDI UBUNGE JIMBO LA SHINYANGA MJINI,ASHINDA KWA KURA 131,126


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobas Katambi, ameibuka mshindi wa nafasi ya Ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Ally Liuye, alitangaza matokeo hayo Oktoba 30, 2025, katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Shycom.

Alimtangaza Katambi kwamba ndiye ameibuka mshindi, baada ya kupata kura 131,126 sawa na asilimia 95.91,dhidi ya wagombea wenzake.
“Natangaza matokeo ya Uchaguzi wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini,Patrobas Katambi wa CCM amepata kura 131,126, Emmanuel Ntobi wa ACT-Wazalendo kura 3,074; Rashid Katabanya wa CHAUMA kura 982; Kitty Juma wa CCK kura 479, Mshandete Lubasha wa CUF kura 425,

“Abdala Sube wa ADA-TADEA kura 153; Clara Maleko wa TLP kura 167; Magreth Sayi wa AAF kura 107; Buliro Venance wa SAU kura 114; na Mnyashi Marwa wa MAKINI kura 88, kwa mamlaka niliyopewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, namtangaza Patrobas Katambi kuwa ndiye mshindi wa kiti cha Ubunge.”amesema Liuye.
Aidha, amesema jumla ya wapiga kura walioandikishwa katika Jimbo la Shinyanga Mjini kuwa ni 147,938, na waliopiga kura watu 136,715, na kwamba hakukuwa na kura iliyoharibika.

Katambi akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, amewashukuru wananchi kwa kumwamini na kumchagua tena kuwa Mbunge wao, na kuahidi kuendeleza kasi ya maendeleo na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi.

Baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani, akiwamo Rashid Katabanya wa CHAUMA, walisema wamekubaliana na matokeo hayo, na kuahidi kumuunga mkono Mbunge Katambi katika hatua zote za maendeleo ya jimbo.

TAZAMA PICHA👇👇
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini Ally Liuye akitangaza matokeo ya Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini Ally Liuye (kulia)akimkabidhi Katambi Hati ya Ushindi kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini Ally Liuye (kulia)akimkabidhi Katambi Hati ya Ushindi kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM,Patrobas Katambi (kulia)akionyesha Hati ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini baada ya kushinda kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29,2025, (kushoto)ni Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha.
Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi akisaini matokeo ya Uchaguzi.
Wagombea wa Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kutoka vyama pinzani wakisaini matokeo ya Uchaguzi.
Aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CHAUMMA,Rashindi Mohamed Katabanya akifurahia kupata kura 982.
Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi akizungumza na waandishi wa habari.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464