` WATANZANIA HAWANA SABABU ZA MSINGI KUANDAMANA, WATUACHE : KAMWAGA

WATANZANIA HAWANA SABABU ZA MSINGI KUANDAMANA, WATUACHE : KAMWAGA

 


Na Mwandishi wetu

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Ezekiel Kamwaga, amesema kwa uwazi kwamba hakuna sababu za msingi zinazoweza kuwafanya Watanzania kuandamana ifikapo Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa hali ya kiuchumi nchini ni tulivu na matumaini ya wananchi yako juu kutokana na mwelekeo thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Kamwaga alisema:“Binafsi siamini kutatokea maandamano Oktoba 29, kwa sababu hakuna matatizo ya kiuchumi yanayosababisha Watanzania kuandamana kama ambavyo tumeshuhudia kwa baadhi ya mataifa jirani. Uchumi wetu uko imara, na wananchi wana imani na Serikali yao.”

Amewataka wale wanaojaribu kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu, akiwemo Mange Kimambi anayejulikana kwa kampeni zake za uchochezi akiwa Marekani, pamoja na Maria Sarungi anayesikika Kenya, kuacha kutumia changamoto ndogo kama kisingizio cha kuwatumia vijana kisiasa.

Kamwaga amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo kuboresha huduma za afya, elimu, ajira, na miundombinu ya kijamii, jambo linaloleta matokeo ya moja kwa moja katika maisha ya wananchi. Ameshauri pia Serikali kuendelea kuwasiliana kwa ukaribu zaidi na wananchi, ikitoa mwelekeo wa maendeleo ya muda mfupi unaoonekana na kuguswa moja kwa moja na jamii.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi, Tanzania inaendelea kudumisha ukuaji wa Pato la Taifa kwa wastani wa zaidi ya asilimia 5.5 kwa mwaka, huku bei za bidhaa muhimu zikiwa katika udhibiti. Hali hii inaifanya nchi kuwa mfano wa uthabiti wa kiuchumi na kisiasa katika Afrika Mashariki.

Kauli hii ya Kamwaga ni ujumbe mzito kwa wapotoshaji wanaotafuta umaarufu mitandaoni kwa ajenda za hofu na taharuki. Tanzania ni nchi salama, yenye uongozi makini, na wananchi wake wanaoendelea kuchagua maendeleo badala ya fujo.

Ukweli ni mmoja; Watanzania hawana muda wa maandamano; wana muda wa kujenga Taifa lao.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464