
Kauli hii inatolewa kufuatia kuwepo kwa upotoshaji wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii, unaodai kuwa mazoezi hayo yanatumika kama vitisho au mbinu za kukandamiza.
Vyombo hivyo vimekiri kuwa kuna propaganda hizo zisizo na msingi zinazoenezwa mtandaoni zinafanywa kwa lengo la kuchochea hofu na kuhalalisha maandamano haramu.
Wito umetolewa kwa wananchi wote kupuuza uzushi wa mitandaoni na kutambua kuwa mazoezi haya ni ngao ya taifa, si tishio kwa wananchi.
"Huu ndio uthibitisho kwamba Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani, salama, na thabiti. Mazoezi haya ni kinga yetu kama taifa," ilihitimisha taarifa hiyo.
Vikosi vya ulinzi vimekumbusha umma kuwa mazoezi ndiyo shughuli yao ya msingi, na hakuna sababu yoyote kwa wananchi kuwa na hofu. Lengo la msingi la mazoezi ya pamoja ni kupima uwezo wa vikosi vyote wakati wa kushughulikia mambo mbalimbali yanayohusu taifa, ikiwamo:Ulinzi wa mipaka na amani ya taifa;Kukabiliana na maafa (mfano: tetemeko la ardhi, mafuriko au majanga mengine) na Kudumisha mshikamano wa kiutendaji kati ya vyombo vyote vya ulinzi.
"Mazoezi haya, yanayojumuisha matembezi ya pamoja, mafunzo ya viungo, na mazoezi ya kivita, yanaboresha afya za askari, yanaongeza weledi wa kazi, na kujenga mshikamano wa kikazi," ilisema taarifa iliyotolewa na vyombo hivyo.
Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimesisitiza kuwa mazoezi mengi hufanyika hadharani katika barabara na maeneo ya wazi ili kuonyesha uwazi na kuhakikisha wananchi wanatambua utayari wa vyombo vyao vya ulinzi.
"Ukweli unabaki palepale: wananchi wengi wameona kwa macho yao kuwa mazoezi haya ni kielelezo cha utayari wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama," ilisisitiza taarifa hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464