Na Mwandishi wetu
Tukiwa tunakaribia Uchaguzi Mkuu, wito mkubwa unatolewa kwa Watanzania wote kulinda hazina yetu ya Amani na Utulivu.
Demokrasia haina maana bila amani. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa, licha ya tofauti zetu za kisiasa, tunadumisha heshima, tunafanya siasa safi, na tunakubali matokeo yanayotokana na sanduku la kura.
Tukumbuke kwamba nchi yetu ni moja, na upigaji kura ni zoezi la muda mfupi, lakini amani ni urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.
Mmoja wa waimbaji wa Injili Christina Shusho ambaye alishawahi kuwa katika kamati ya Amani nchini Tanzania wakati wa Utawala wa awamu ya nne anasema kwamba kila siku ni lazima wananchi lazima watambue umuhimu wa uhai na kuenzi Amani.
Anasema ni kazi kubwa kuenzi Amani lakini ni rahisi kubomoa kama watu hawatakuwa waangalifu katika kauli na matendo yao na kwamba bila Amani hakuna shughuli nyoiyote itakayostawi.
Uchaguzi Sio Vita, Ni Maamuzi
Ni muhimu kwa Vyama vya Siasa na Wafuasi wao kuweka mbele maslahi ya Taifa. Uchaguzi si vita, bali ni mchakato wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi tunaowaamini. Badala ya kuruhusu jazba na chuki, tunapaswa kujikita katika hoja, mijadala yenye tija, na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi vimeapa kulinda raia na mali zao, na vinahitaji ushirikiano wetu ili kudumisha utulivu katika kipindi chote cha kampeni, upigaji kura na baada ya matokeo. Tutumie fursa hii ya kidemokrasia kwa ustaarabu na utulivu.
Jukumu la Kiongozi na Mwananchi
Viongozi wa kisiasa wanalo jukumu la kutoa hotuba zenye kuhamasisha umoja na kuacha kauli zinazochochea mgawanyiko au vurugu. Kadhalika, kila mwananchi anawajibika kuepuka kueneza taarifa za upotoshaji (fake news) au uchochezi kupitia mitandao ya kijamii. Amani huanzia kwetu.
Kanisa Katoliki kupitia viongozi wake wakuu akiwemo Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Dar es Salaam Thadeus Ruwaich amesisitiza wananchi kutoyumbishwa na taarifa zisizo sahihi na kwamba kanisa halina ugomvi na serikali na ni vyema wananchi wakatimiza sharia zilizopo.
Kwa kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inakwenda kwa utulivu, Watanzania wanapaswa kutoaa heshima kwa katiba ambayo ndiyo inaweka msingi thabiti wa maendeleo endelevu. Tanzania itabaki salama na imara ikiwa wananchi wataweka kura zao kama haki yao, na amani kama wajibu wao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464