Kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Shinyanga mjini imefanya ziara ya ya kutembelea vijiwe vya wauza Kahawa katika kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga kwa kuomba kura, za chama cha Mapinduzi CCM .
Ziara hiyo imefanyika leo katika maeneo ya mtaa wa Banduka na mtaa wa Ndala senta iliyoongozwa na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Fue Mrindoko,akiambatana na katibu wake Doris Kibabi, ambapo imejumuika na wananchi wa kata hiyo kwa kunywa kahawa na kuwaomba wakipigie chama cha mapinduzi CCM.
"Mimi na kamati yangu ya utekelezaji nimekuja hapa kwa ajili ya kuwakumbusha tu kwamba tarehe 29 yaani kesho kutwa tuamke mapema tuhamasishe vijana wetu marafiki zetu twende tukapige kura, tusipotoshwe na baadhi ya wapotoshaji wanaosema kuna maandamano, hakuna maandamo yoyote kutakuwa na amani tu tukawapigie diwani, mbunge na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan,"amesema Mrindoko.
Katibu elimu na malezi Richard. Mseti amesema siku ya uchaguzi kutakuwa salama kwa sababu serikali iko kazini kuhakikisha kila. mwananchi anakuwa salama hivyo wajitokeze kupiga kura wasiwe na hofu
Mjumbe wa kamati ya utekelezaji Boniphace Giti amewaomba wananchi kuachana na imani za maandamano wanazopandikizwa wanatakiwa waiamini serikali kuwa itaweka usalama wa kutosha hivyo waende asubuhi kuanzia saa moja vituo vitakuwa vimefunguliwa wanapiga na kurudi nyumbani.
"Tuwaambie vijana wetu wasithubutu kuandamana, kwani sisi watanzania hatujalelewa kwa kuandamana, niwaombe tu kwamba tukiamka asubuhi tukapige kura kwa amani na kurudi nyumbani, na kila mtu ana haki ya kupiga kura,hivyo tuwasaidie wazee tuwaelekeze maeneo ya kupigia kura wakakipigie chama cha mapinduzi CCM.
Kwa upande wake mgombea wa udiwani kata ya Ndala Zamda Shaban. amesema yeye wakati akiwa diwani wa kata hiyo ameshirikiana na mbunge wa jimbo hilo Patrobas Katambi wamefanya maendeleo makubwa katika katika kata ya Ndala, ambapo aliibua shule ya Msufini B na maenndeleo mengine mengi kwa kushirikiana na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Tumefanya makubwa lakini tumejipanga vizuri katika kuleta maendeleo katika kata hii ya Ndala, tunahitaji zahanati na kufanya mambo mengibe, hivyo naombeni kura zenu ili niendelee kuwatumikia tutoke tulipoishia tufanye makubwa zaidi"amesema Zamda.
Nao baadhi ya wananchi walioshiriki kunywa kahawa kwenye vijiwe hivyo wamesema wanawashukuru kwa kuwatembelea, wao bado wanakiamini chama cha mapinduzi CCM, hivyo wako tayari kwenda kupiga kura tarehe 29.
"Mimi mwenyewe nimefurahishwa sana na jumuiya hii kwa kutukumbuka na sisi watumia kahawa hivyo nitahamasisha marafiki zangu na nitatoka na familia yangu kwenda kumpigia diwani wangu Zamda Shaban, mbunge wangu Patrobas Katambi na Rais Samia Suluhu ili waendelee kututumikia, ila niombe tukiwachagua tu barabara yetu ya kwenda Mwawaza muitengeneze kwa haraka ili kuepula vumbi"amesema Charles Chacha.
Aidha Katibu wa jumuiya ya wazazi Shinyanga mjini Doris Kibabi amewaomba wananchi wote wa wilaya ya Shinyanga mjini wasidanganyike wajitokeze wote kukipigia chama cha mapinduzi CCM, ili kiendelee kuwatumikia wananchi kwa amani na utulivu
"Ndugu zangu leo tumebakiza siku moja tu tukapige kura niwaombe ndugu zangu tusiwe na hofu, tuyapuuze maneno yote ya wapotoshaji hivyo tuamke mapema tukampigie mama yetu Samia Suluhu Hassan, mbunge wetu Patrobas Katambi na Diwani wetu wa kata hii Zamda Shaban, halafu turudi ndani tutulie,"amesisitiza Kibabi.