Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Joseph Sahani Swalala akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura Oktoba 52,2025 katika Ukumbi wa Stage II Hoteli wilayani humo
Na Sumai Salum-Kishapu
Katika kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unaendeshwa kwa weledi, uwazi na uadilifu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga imeendesha mafunzo maalum kwa watendaji wa uchaguzi wakiwemo makarani waongozaji wapiga kura kutoka katika Kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Oktoba 25 Ukumbi wa Stage II Hotel ni sehemu muhimu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao Oktoba 29,2025 yakilenga kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo yaliyowekwa.
Kujenga Uelewa na Uadilifu
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo Hilo Joseph Sahani Swalala ambae ni mwakilishi wa Tume amesisitiza umuhimu wa watendaji wa uchaguzi kutambua dhamana kubwa waliyonayo kwa taifa, akieleza kuwa kazi ya kusimamia upigaji na kuhesabu kura ni jukumu nyeti linalohitaji uaminifu, umakini na uzingatiaji wa maadili ya kazi za umma.
“Dhamana mliyopewa ni kubwa na muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu. Hivyo, mnatakiwa kufuata sheria, kanuni na maelekezo yote mtakayopatiwa hadi kukamilika kwa jukumu hili muhimu la Uchaguzi Mkuu,” amesema Swalala.
Jumla ya makarani 614 wameshiriki katika mafunzo hayo kutoka vituo 556 vilivyopo katika kata 29 za Halmashauri ya Kishapu. Washiriki hawa ni makarani waongozaji wapiga kura watakaosimamia shughuli za upigaji na kuhesabu kura katika vituo vyao husika.
Kupitia mafunzo haya, watendaji hao wamepata nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi, na kujifunza mbinu bora za kuhakikisha zoezi linakuwa huru, wazi na lenye amani na Kukuza Ujuzi na Uzoefu
Kwa wale wanaoshiriki kwa mara ya kwanza
Wamekumbushwa kuwa Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua kadhaa za kikatiba na kisheria, na kwamba kila hatua inapaswa kufuatwa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha matokeo ya mwisho yanakuwa sahihi, halali na yanayokubalika na pande zote.
“Hatua na taratibu hizi ndizo msingi wa uchaguzi huru na wa haki, ambao hupunguza au kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi,” amesisitiza
Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo Mgeni rasmi, Bi. Mona S. Bitakwate, amewataka watafsiri mafunzo hayo kwa kuhusianisha na zoezi la upigaji kura. Amesema kuwa mafunzo haya yamewajengea uwezo washiriki na kuwakumbusha umuhimu wa kutunza siri, kwa mujibu wa kiapo walichoapa chini ya sheria. Pia amewasisitiza kupunguza matumizi ya makundi ya WhatsApp ili kuepuka makosa yatakayoweza kusababisha taarifa za siri kuvuja.
Aidha, amehitimisha kwa kusisitiza kufuata muda wa kufungua na kufunga vituo vya kupigia kura, kufanya kazi kwa uzalendo na weledi, kushirikiana vizuri kazini, kutumia lugha nzuri, na kuwapa kipaumbele wapiga kura wenye mahitaji maalum watakapofika vituoni.
Kwa ujumla, mafunzo haya ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Tume ya Uchaguzi kuandaa watendaji wake kwa ufanisi, kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inatekelezwa kwa weledi na uadilifu. Huu ni msingi imara wa kujenga uchaguzi huru, haki na wenye kuaminika — nguzo muhimu ya demokrasia ya Tanzania.
Mgeni rasmi wa uzinduzi wa mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mona S. Bitakwate akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo 52,2025 katika Ukumbi wa Stage II Hoteli wilayani humo
Afisa Uchaguzi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Sigisbert M. Rwezaula akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura Oktoba 52,2025 katika Ukumbi wa Stage II Hoteli wilayani humo
Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Kishapu Mkoani
Shinyanga Feada Mbilinyi akitoa elimu ya Makosa ya Rushwa kipindi cha uchaguzi kwenye mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura Oktoba 25,2025 ukumbi wa Stage II Hotel Wilaynai humo
Mwezeshaji wa mada ya kwanza iliyohusu Wajibu na majukumu ya makarani waongozaji wapiga kura Nkinga Daudi Mgoyeji
Mwezeshaji mada ya pili iliyohusu namna ya kuwapokea na kuwaongoza wapiga kura katika kituo cha kupiga kura Elizabeth Jospeh Simbaih