` KATAMBI AHITIMISHA KAMPENI KWA KISHINDO,AWAOMBA WANANCHI WAMPE MITANO TENA

KATAMBI AHITIMISHA KAMPENI KWA KISHINDO,AWAOMBA WANANCHI WAMPE MITANO TENA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Patrobas Katambi, amehitimisha kampeni kwa kishindo kwa kunadi sera na Ilani ya CCM,huku akiwaomba wananchi wamwamini na kumtuma tena kwa awamu nyingine ya miaka mitano ili aendelee kuwaletea maendeleo.
Kampeni hizo zimefungwa leo Oktoba 25,2025, katika viwanja vya Relini, na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga.

Katambi, akihutubia wananchi hao, amewataka kujitokeza kwa wingi siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 kumpigia kura za ushindi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, madiwani wa CCM, pamoja na yeye mwenyewe,ili waendelee kuwaletea maendeleo.
“Siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 hakutakuwa na maandamano. Wananchi jitokezeni kwa wingi mkapige kura na kuwachagua viongozi wote wa CCM ambao ndio watawaletea maendeleo,” amesema Katambi.

Akimzungumzia Rais Dk. Samia, Katambi amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, licha ya kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa na Hayati Dk. John Magufuli, amefanikisha utekelezaji wa miradi hiyo ukiwemo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Bomba la Mafuta, Daraja la Magufuli, na Viwanja vya Ndege ikiwemo ule wa Ibadakuli,Shinyanga.
“Miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa na Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan. Hii niliyotaja ni baadhi tu, tukisema yote tutakesha hapa. Shukrani pekee tunayoweza kumpa ni kumpigia kura nyingi za ushindi Oktoba 29 ili aendelee kuwa Rais wetu kwa miaka mingine mitano,” alisema Katambi.

Kwa upande wa miradi iliyotekelezwa katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Katambi amesema sekta ya elimu wamejenga shule mpya 11 (Msingi 6 na Sekondari 5), pamoja na vyumba vya madarasa, maabara, mabweni na kuboresha upatikanaji wa vyuo vikuu.
Katika sekta ya afya, amesema wamekamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa iliyopo Mwawaza, kujenga zahanati mpya nane, nyumba za watumishi, kununua vifaa tiba vya kisasa na magari ya kubebea wagonjwa (ambulance).

Ameahidi kuwa, endapo atapewa ridhaa tena, watajenga vituo vipya vya afya vitano, na sasa wanajenga pia stendi mpya ya mabasi ya mkoa, na kuboresha barabara za lami ikiwemo ile inayoelekea hospitali ya mkoa.
Aidha, amewataka madiwani wa CCM kwamba wakawe waadilifu, wenye kujali maslahi ya wananchi na kusimamia utekelezaji wa ahadi na miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anold Makombe, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi, na kuwachagua wagombea wote wa CCM, ili waendelee kuwaletea maendeleo.

TAZAMA PICHA👇👇
Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM Patrobas Katambi akinadi sera kwa wananchi wakati wa kuhitimisha kampeni zake.
Mwenyeki wa Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga Jonh Siagi akizungumza.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza.
Mwenyekiti wa CCM Wwilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464