` DAR INAPOJIANDAA KUWA ‘MEGA CITY’: KURA YAKO NI MUHIMU

DAR INAPOJIANDAA KUWA ‘MEGA CITY’: KURA YAKO NI MUHIMU

Kila mara tunapokaribia uchaguzi, mijadala hujawa na mbwembwe, matusi na maneno matupu yanayopoteza muda. Lakini Uongozi wa kweli sio makelele jukwaani; ni uwezo wa kutafsiri maono makubwa kuwa matendo halisi yanayoleta maendeleo na fursa za ajira kwa wananchi. 

Huu ndio wakati wa kuingia kwenye sanduku la kura kuamua mabadiliko kwa kutambua kiongozi anayesema ukweli unaogusa mahitaji yetu ya msingi na anayeweza kusimamia mabadiliko yaliyokusudiwa.

Kiukweli, kura yako ni muhimu sana kwani inatoa mamlaka ya kusimamia mabadiliko makubwa ya Taifa hili. Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania inaendelea kuandika historia mpya ya maendeleo kupitia miradi mikubwa ya usafiri wa kisasa na kazi hii inahitaji usimamizi wa karibu. 

Baada ya mafanikio makubwa ya Reli ya Kisasa (SGR) inayotumia umeme, sasa macho ya Watanzania yanaelekezwa kwenye hatua nyingine kubwa zaidi ya kuboresha miundombinu ya usafiri.

Mtaalamu wa Miundombinu, Bw Salum Mturi, anasisitiza: "Kama hatutapiga kura kwa kiongozi mwenye maono ya miundombinu, tutabaki kwenye foleni kwa miaka mingine mitano. Kura yetu ndiyo inahakikisha Serikali inaendelea na kasi hii."

Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mpango uko tayari wa kuanza ujenzi wa treni za mijini (Metro) katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha maisha ya wananchi kwa kupunguza msongamano, kurahisisha usafiri, na muhimu zaidi, kukuza uchumi wa mijini.

Wakati Dar es Salaam inajiandaa kuwa “megacity” ya kwanza Afrika Mashariki yenye wakazi zaidi ya milioni 10, Mradi wa Metro na ujenzi wa miundombinu inayouzunguka unahakikisha ukuaji huu wa watu unakwenda sambamba na ufanisi wa usafiri. Huu si tu ujenzi wa miundombinu; ni injini ya kutoa ajira kulingana na mahitaji yetu halisi.

Maeneo kama Morocco, Mwenge, Magomeni na Tabata yanatarajiwa kupata barabara za juu (flyovers), ambayo yanatarajiwa kujengwa barabara hizo yanamaanisha kazi nyingi za ujenzi, uhandisi, na usimamizi. 

Bi. Neema John, mhitimu wa Uhandisi (25), anasema: "Miradi mikubwa kama flyovers na Metro inamaanisha ajira kwetu. Mimi sitapiga kura kwa maneno matupu, nitapiga kura kwa yule anayeonesha wazi mahali pa kwenda kufanya kazi."

Kila mradi unaotekelezwa, ukiwemo wa Arena (ukumbi mpya wa kimataifa utakaobeba watu 15,000) katika eneo la Kawe, unatafsiriwa kuwa fursa mpya za ajira ndogondogo na uwekezaji katika sekta binafsi.

Kama ilivyokuwa ndoto kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa saa moja kupitia SGR, sasa treni za Metro zitakuwa ishara ya zama mpya za ufanisi na teknolojia. Huu ndio ukweli tunaokubaliana nao kama mahitaji yetu.

Acha Mbwembwe

Wakati wa kupiga kura, acha kupoteza muda na mbwembwe na badala yake, angalia matokeo ya kazi. Kura yako lazima iwe kwa dira ya maendeleo, kasi, na uthubutu ambayo inajibu moja kwa moja mahitaji ya ajira na maisha bora ya mwananchi.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464