MKURUGENZI WA MALULA TV AHUDHURIA MAHAFALI YA DARASA LA SABA SHULE YA MSINGI SHATIMBA
SHINYANGA
Shule ya Msingi Shatimba leo imefanya mahafali ya wahitimu wa darasa la saba mwaka 2025 kwa shamrashamra na burudani mbalimbali, huku mgeni rasmi akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Malula TV, ambaye alipokelewa kwa heshima kubwa na uongozi pamoja na wanafunzi wa shule hiyo.
Katika risala ya wahitimu,wanafunzi walitoa historia fupi ya shule ya Msingi Shatimba ambayo ilianzishwa rasmi tarehe 18/11/1975, ikianzia na wanafunzi wachache na sasa ikiwa na zaidi ya wanafunzi 852. Aidha, shule hiyo imeendelea kutoa elimu bora licha ya changamoto mbalimbali za miundombinu.
Wahitimu hao walieleza kuwa mwaka huu wa 2025 idadi ya wanafunzi wanaohitimu ni 54, wakiwemo wavulana 33 na wasichana 21. Risala ilionyesha pia matokeo ya ufaulu katika miaka ya hivi karibuni ambapo ufaulu umeendelea kuimarika, ikiwemo mwaka jana wa 2024 ambapo wanafunzi 36 kati ya 40 walifaulu, sawa na asilimia 92.
Wanafunzi walitumia risala yao pia kueleza changamoto za shule ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa, upungufu wa vitabu, pamoja na uwanja wa michezo. Walisema bado kuna uhitaji wa kusaidia ujenzi wa madarasa mapya pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia.
Akizungumza mara baada ya risala hiyo, Mkurugenzi wa Malula TV aliwapongeza wanafunzi wote kwa hatua hiyo muhimu ya kitaaluma na kuwataka watumie elimu waliyoipata kama msingi wa kufanikisha ndoto zao. Aliahidi kushirikiana na uongozi wa shule hiyo pamoja na wadau wengine wa elimu katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi.
"Elimu ndiyo nyenzo pekee ya kumtoa mtoto katika giza la ujinga na kumuweka kwenye mwanga wa maarifa. Wahitimu hawa mnapaswa kuwa mfano wa nidhamu, bidii na heshima ili muweze kufanikisha maisha yenu ya baadaye," alisema Mkurugenzi wa Malula TV
Hata hivyo mgeni Rasmi aliwasihi wazazi kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wa kike pindi wamalizapo elimu ya darasa la Saba na kuwaomba wazazi kuwapa ushirikiano watoto hao ili watimize ndoto zao
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na walimu, wazazi, pamoja na viongozi wa kijamii waliokuwa na furaha kubwa kushuhudia watoto wao wakihitimu elimu ya msingi.