Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amewahakikishia wananchi kuwapo kwa usalama siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, na kuwasihi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura.
Mtatiro ametoa kauli hiyo leo Oktoba 27, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo amesema Wilaya ya Shinyanga ipo salama na hakuna viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.
“Nawaomba wananchi wasitishwe na taarifa zinazozagaa mitandaoni kwamba siku ya uchaguzi kutakuwa na maandamano. hicho kitu hakipo, bali amani itatawala na wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka,” amesema Mtatiro.
Ameongeza kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi usifanyike kwa kuwa ni takwa la kikatiba, na kwamba mtu yeyote au kikundi kitakachojaribu kufanya vurugu siku hiyo kitapambana na mkono wa dola.
Aidha, Mtatiro amewahakikishia watu wenye ulemavu, wazee na wanawake wenye watoto wadogo kuwa watapewa kipaumbele wakati wa kupiga kura.
Ametaja idadi ya vituo vya kupigia kura wilayani humo kuwa ni 1,007, ambapo Jimbo la Shinyanga Mjini lina vituo 391, Solwa vituo 364 na Itwangi vituo 252.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utafanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Watanzania watapiga kura kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais.