Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupata uchunguzi, ushauri na matibabu ya kibingwa kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Mama Samia, waliopiga kambi ya siku tano mkoani humo.
Mhita ametoa wito huo leo Oktoba 13,2025 wakati wa kuwapokea Madaktari Bingwa 36 waliowasili mkoani humo, ambao wamesambazwa katika halmashauri zote sita za mkoa huo.
Amesema madaktari hao wamekuja kwa lengo la kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi, hivyo ni fursa kwa wakazi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma hizo.
“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi kwenye kambi hii ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia, ambao wameweka kambi kwa muda wa siku tano mfululizo ili kufanya uchunguzi, kupata ushauri na matibabu ya kibingwa,” amesema Mhita.
Amesema,Madaktari hao Bingwa pia wamekuwa wakiwajengea uelewa wananchi kwa kuondokana na Imani za kishirikina kupitia matibabu,kwamba kama kuna mtu alikuwa akiamini huenda ugonjwa wa mtoto wake unatokana na kurogwa ndiyo maana haponi,lakini akipata matibabu ya kibingwa na kupona Imani hiyo inatoweka.
Aidha,amesema hiyo ni awamu ya Nne sasa Madaktari hao Bingwa wa Mama Samia wanaweka kambi mkoani humo, na kwamba hadi sasa wameshatoa matibabu kwa wananchi 240,000, kujengea uwezo Wataalamu wa Halmashauri 15,000.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kambi hiyo Michael Mbele, amesema wamejipanga vyema kutoa huduma bora kwa wananchi wa Shinyanga, na wanatarajia kuwafikia zaidi ya watu 30,000 katika kipindi hicho cha siku tano.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye ujio wa Madaktari Bingwa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa Michael Mbele akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464