Na Mwandishi Wetu
ALIYEKUWA mgombea wa Udiwani Kata ya Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rahma Petro Kware, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kumpigia kura ya ndiyo Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea wengine wa chama hicho ngazi ya ubunge na udiwani.
Akizungumza jana mjini Shinyanga, Rahma alisema CCM ni chama kinachoongozwa kwa misingi ya umoja na mipango madhubuti, na si ushindani wa ndani, bali maandalizi ya kupeperusha bendera ya chama kwa maslahi ya wananchi.
“Kwenye Chama Cha Mapinduzi hatushindani, tunajipanga. Tumejipanga vizuri, na mmoja wetu amepewa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama chetu. Huyo ndiye chaguo letu sote,” alisema Rahma.
Aliongeza kuwa kama Mtanzania mzalendo na mwanachama halali wa CCM, anaipongeza Serikali kwa kuleta wagombea imara katika ngazi zote za uongozi, akisema ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuendeleza dira ya maendeleo ya chama hicho.
Amsifia Rais Samia kwa utendaji na maono
Rahma alisema tangu kuingia madarakani mwaka 2021, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uongozi imara, hekima na busara, licha ya kuchukua nchi katika kipindi kigumu baada ya kifo cha hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
“Rais wetu hakutetereka. Amesimama imara na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake, ikiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, ujenzi wa Makao Makuu Dodoma, reli ya kisasa ya SGR na Daraja la Magufuli,” alisema Rahma.
Alisema Rais Samia pia ameibua falsafa ya R4 inayojikita katika Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Taifa, ambayo imechangia kudumisha umoja, amani na maendeleo nchini.
Rahma aliongeza kuwa Rais Samia amegusa sekta nyingi ikiwemo umeme, maji, elimu, afya, nishati, madini, biashara na viwanda, jambo linalothibitisha uwezo wake wa kiutawala na kiu ya maendeleo kwa Watanzania.
Aeleza vipaumbele vya siku 100
Aidha, Rahma alinukuu baadhi ya vipaumbele vya Rais Samia kwa siku 100 za mwanzo endapo atachaguliwa tena, ikiwemo kuboresha sekta ya elimu, afya, ajira na kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema katika sekta ya afya, Rais Samia ameahidi kuzindua Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, ambao utaanza kwa awamu ya majaribio na kugharamia matibabu ya makundi maalumu kama wazee, watoto, mama wajawazito na watu wenye ulemavu.
Pia ametaja mpango wa kutenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na kampuni changa, pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ikiwemo mama lishe, bodaboda, bajaji na wajasiriamali wadogo ili waweze kunufaika na huduma rasmi za Serikali.
Atoa mwito wa kujitokeza kupiga kura
Rahma aliwataka Watanzania, hususan vijana na wanawake, kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura kwa Rais Samia, wabunge na madiwani wa CCM, akisema ni njia sahihi ya kuendeleza amani, utulivu na maendeleo nchini.
“Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, nawaomba Watanzania wenzangu, baba, mama na vijana wenzangu, ifikapo Oktoba 29 twendeni tukapige kura zetu za ndiyo. Kidumu Chama Cha Mapinduzi, kidumu uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Rahma.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
