Mgombea ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete, ashiriki mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Mihuga, Kata ya Miono, Halmashauri ya Chalinze, ikiwa ni sehemu ya kuendelea kunadi sera na kuwaombea kura wagombea wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Katika hotuba yake kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo, Riziwani Kikwete aliwataka wananchi kuendelea kuiamini CCM na kumuunga mkono mgombea wa Urais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa serikali yake imeleta mafanikio makubwa na ya kihistoria katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
“Ninawasihi sana ndugu zangu wa Chalinze, tuendelee kushikilia imani yetu kwa CCM na kwa Rais wetu Dkt. Samia. Yeye ni kiongozi wa vitendo, na Ilani ya CCM imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa chini ya uongozi wake,” alisema Ridhiwani.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wote kutoka CCM yaani Diwani, Mbunge na Rais maarufu kama mafiga matatu, akieleza kuwa mshikamano wa viongozi kutoka chama kimoja ndio siri ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Ushirikiano na maelewano baina ya viongozi wa chama chetu ndio unaofanikisha kasi kubwa ya maendeleo. Tukichagua mafiga matatu kutoka CCM, tunaipa nafasi serikali kuendelea na kazi iliyoanza,” aliongeza.
Ridhiwani pia alitumia nafasi hiyo kuzungumza na makundi ya vijana na wanawake, akiahidi kwamba atahakikisha fursa za kiuchumi, ajira, na uwezeshaji wa vikundi maalum zinaimarishwa zaidi iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Chalinze.