` MAHAFALI YA CHEKECHEA 'PRE UNIT' NA DARASA LA SABA 2025 SHULE YA LITTLE TREASURES YAFANA

MAHAFALI YA CHEKECHEA 'PRE UNIT' NA DARASA LA SABA 2025 SHULE YA LITTLE TREASURES YAFANA

 

Shule ya Msingi na Awali Little Treasures iliyopo kijiji cha Bugayambelele, kata ya Kizumbi, manispaa ya Shinyanga, imefanya mahafali ya 14 ya chekechea na ya 9 ya darasa la saba kwa furaha kubwa na shamrashamra.

Mahafali haya yalihusisha jumla ya wahitimu 164, ambapo 65 walikuwa wa chekechea na 99 kutoka darasa la saba. 

Wahitimu wametunukiwa vyeti vyao baada ya kukamilisha masomo kwa mafanikio makubwa.

Wakisoma risala ya shule, wanafunzi wameeleza kuwa Little Treasures imekuwa ikitoa huduma bora kwa watoto ikiwemo usafiri wa uhakika, mabweni ya kisasa, walimu wenye sifa za kitaaluma, chakula bora na mazingira salama ya kujifunzia.

Aidha, shule inajivunia kuwa karibu na Luckmed Polyclinic, hospitali iliyoko mita 500 kutoka shuleni, ambayo inatoa huduma za afya si kwa wanafunzi pekee bali pia kwa jamii inayozunguka. Hii imehakikisha usalama na afya ya watoto inabaki kipaumbele cha shule.

Mgeni rasmi wa mahafali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mheshimiwa Julius Mtatiro lakini aliwakilishwa na Mthibiti Ubora wa Shule, Samson Nyanda.

Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Nyanda ameipongeza Little Treasures kwa malezi bora na mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, *Lucy Mwita*, amewahimiza wahitimu kuendelea kujituma na kutumia elimu kama silaha ya kufanikisha ndoto zao.

> “Kwa watoto wetu wa chekechea, leo mmeweka msingi muhimu wa safari yenu ya elimu. Kwa wahitimu wa darasa la saba, mmehitimu hatua kubwa ya maisha yenu na sasa mnaelekea sekondari. Elimu ndiyo silaha yenu ya kupambana na changamoto za maisha,” amesema Lucy.

Aidha, Lucy amewapongeza walimu na wazazi kwa ushirikiano na kujitoa kwao, huku akisisitiza mshikamano baina ya shule, wazazi na jamii katika kulea watoto.

Shule hiyo ya Sekondari imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma, ambapo mwaka jana kati ya watahiniwa 58 wa kidato cha nne, 41 walipata Division One na 17 Division Two.

Sherehe zilipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo nyimbo, ngoma na michezo ya kisanaa iliyoandaliwa na wanafunzi.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464