Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Acksonakimtambulisha Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe Lucy Thomas Mayenga(kulia) Septemba 19,2025 katika Viwanja vya Mabela Wilayani Kishapu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson, amefanya ziara Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga ambapo amezungumza na Wananchi kuhusu mipango ya maendeleo iliyomo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030.
Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika Septemba 19,2025 katika Viwanja vya Mabela, Spika Tulia amewataka Wananchi wa Kishapu kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu ujao, akibainisha kuwa ni njia pekee ya kuchagua viongozi wanaowaamini kuwaletea maendeleo.
"Ndugu zangu wa Kishapu Ilani ya CCM imebainisa mambo mengi mtakayonufaika nayo wakazi wa eneo hili hasa changamoto yenu ya Barabara ya Kolandoto -Mhunze Itatengenezwa Kwa kiwango Cha lami ili kuongeza kipato Kwa Wananchi kutokana na kufanya Kazi bila kikwazo Cha miundombinu" amesema Tulia
Katika hotuba yake, Spika Tulia amewafikishia wananchi salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwashukuru kwa uvumilivu wao na namna wanavyoendelea kuiamini Serikali katika kusimamia maendeleo ya Taifa.
Aidha, amewaahidi wananchi wa Kishapu kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya, kuimarisha miundombinu ya barabara, kuinua kiwango cha elimu, kupeleka huduma za maji safi na salama, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa umeme Kwa kila Kitongoji na unaongezeka.
Mhe. Tulia amewatambulisha rasmi kwa Wananchi,Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kishapu kupitia CCM, Mhe. Lucy Thomas Mayenga, pamoja na wagombea udiwani wa Kata zote 29 zinazounda Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akizungumza baada ya utambulisho huo, Mhe. Lucy Mayenga amekishukuru Chama Chake kwa imani waliyoonyesha kwake kwa kumpa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM. Ameahidi kuwa endapo Wananchi watampa ridhaa ya kuwa Mbunge wao, atahakikisha analeta maendeleo yenye tija yanayogusa maisha ya kila mmoja.
“Nataka niwahakikishie Wananchi wa Kishapu, nikipewa nafasi ya kuwa mwakilishi wenu, nitashirikiana nanyi bega kwa bega kuhakikisha huduma bora za jamii zinapatikana kwa wakati na miradi ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo,” amesema Mayenga.
Vilevile, Mhe. Lucy Mayenga amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, kwa usimamizi mzuri ndani ya Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bw. Emmanuel Johnson, kwa kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ziara ya Spika Tulia Akson Kishapu imeendelea kuongeza hamasa ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ifikapo Oktoba 29 ambapo wananchi wamehimizwa kushiriki kwa amani na mshikamano.



Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 19,2025 katika Viwanja vya Mabela.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464