` MHE.SAUM WA UDP AUNGURUMA KISHAPU ANADI VIPAUMBELE VYA KUMKOMBOA MTANZANIA

MHE.SAUM WA UDP AUNGURUMA KISHAPU ANADI VIPAUMBELE VYA KUMKOMBOA MTANZANIA

Mgombea Urais Kwa tiketi ya Chama Cha United Democratic Party (UDP) Mhe.Saum Hussein Rashid akizungumza wakati akinadi sera za Chama hicho alipokuwa kwenye viwanja vya Stendi ya zamani Mhunze,Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025

Na Sumai Salum – Kishapu

Mgombea Urais kupitia Chama cha United Democratic Party (UDP), Mhe. Saum Hussein Rashid, ametangaza ajenda kuu ya vipaumbele sita ambavyo chama chake kitatekeleza endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akihutubia mamia ya Wananchi katika Viwanja vya Stendi Ndogo Mhunze, Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, Septemba 15,2025 Mhe. Saumu amesema sera za UDP zinalenga kumwinua Mtanzania mmoja mmoja na kuimarisha uchumi wa taifa zima kupitia rasilimali zilizopo.


Amebainisha kuwa vipaumbele hivyo ni miundombinu ya barabara, elimu, afya, maji, kilimo na umeme, akieleza kuwa sekta hizo ndizo nguzo kuu za ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza kuhusu kilimo, ameeleza kuwa kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, serikali ya UDP itaanzisha mabwawa makubwa ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa mvua. Amesema hatua hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa taifa linalojitosheleza kwa chakula na kufungua fursa za kibiashara ndani na nje ya nchi.

Mhe. Saumu amesema elimu ndiyo msingi wa maendeleo, hivyo chama chake kitaweka mkazo katika kuhakikisha wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi chuo kikuu wanapata fursa sawa za masomo Kwa kutochangia gharama zozote.

Ameahidi iwapo Chama chake kitapata ridhaa ya kuingia madarakani kutakuwa na mfumo wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana,Wanawake na watu wa makundi maalumu ili kuwawezesha kupata Kwa liba nafuu.


Mgombea Mwenza Chama Cha United Democratic Party (UDP) Mhe. Juma Khamis Fack akizungumza alipokuwa na Mgombea Urais wa Chama hicho Mhe. Saum Hussein Rashid wakati wakinadi sera za Chama hicho Viwanja vya Stendi ya zamani Mhunze,Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025

Katika sekta ya afya, ameeleza dhamira ya UDP ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata bima ya afya yenye gharama nafuu, sambamba na kuboresha miundombinu ya hospitali, kuongeza vifaa tiba na wahudumu wa afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi kote nchini.

Akizungumzia huduma za kijamii, amesema barabara, maji safi na nishati ya umeme vitapewa kipaumbele maalum kwani ndio msingi wa uwekezaji, biashara na ustawi wa maisha ya wananchi, hasa Vijijini.

Mgombea huyo amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa, akiwataka wananchi kufanya maamuzi kwa mujibu wa sheria bila kushawishiwa na ahadi zisizo na tija.

“Baada ya uchaguzi maisha lazima yaendelee, hivyo tuendelee kulinda amani yetu na kuchagua viongozi tunaowaamini,” amesema Mhe. Saum.

Mbali na hayo amewakumbusha Wananchi kuwalinda na kuwajari watu wenye mahitaji maalum kwa kuondokana na Mila na desturi potofu huku wakiweka kando itikadi zao za kidini,siasa na ukabila kwani Kwa kufanya hivyo ni kulinda haki zao za Msingi.


Katibu Mwenezi wa Chama Cha Democratic Party Taifa (UDP) Nyaga Susani akizungumza kwenye mkutano huo wa kusaka kura kwa wananchi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025

Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa UDP, Mhe. Juma Khamis Fack, amewaomba wananchi wa Tanzania kutofanya makosa ifikapo siku ya kupiga kura, bali wawape nafasi ili waweze kuleta mageuzi yanayolenga kumkomboa Mtanzania wa kawaida kiuchumi na kijamii.

Mhe.Saum ataendelea na ziara yake ya kunadi sera za UDP kwa kusaka kura za Wananchi kuelekea Ikulu ifikapo Oktoba 29,2025 ambapo Kesho Septemba 16,2025 atakuwa na mkutano Wilayani Kahama.

Katibu KinaMama Taifa Chama Cha Democratic Party (UDP) Stella John Cheyo akizungumza kwenye mkutano huo wa kusaka kura kwa wananchi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025 
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic Party (UDP) Machimu Maige akizungumza kwenye mkutano huo wa kusaka kura kwa wananchi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025







Mgombea Urais Mhe.Saum Hussein Rashid (Kushoto) na Mgombea mwenza Mhe. Juma Fack (Kulia) kwa tiketi ya Chama Cha United Democratic Party (UDP) wakiwa Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025




































Mgombea Urais Mhe. Saum Hussein Rashid na Mgombea Mwenza Mhe. Juma Fack wa Chama Cha United Democratic Party (UDP) wakipiga picha ya pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu waliokuwa kwenye uwanja wa Stendi ya Zamani Mhunze, Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Septemba 15,2025




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464