` HOROHORO AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA

HOROHORO AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA

 


Dar es Salaam, 23 Septemba 2025

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi, imemhukumu Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Horohoro” kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 326.46.

Hukumu hiyo ilisomwa tarehe 23 Septemba 2025 na Mheshimiwa Jaji S.E. Kisanya, baada ya kusikiliza mashahidi 14 na kupitia vielelezo 23 vilivyowasilishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa ushahidi, Horohoro alikamatwa tarehe 31 Oktoba 2023 katika eneo la Boko Magengeni, Kinondoni – Dar es Salaam, akiwa anaendesha gari aina ya BMW X5 lenye namba za usajili T189 DWY. 

Ndani ya gari hilo, maafisa wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) walipata mfuko mwekundu wenye unga uliothibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kuwa ni cocaine yenye uzito wa gramu 326.46.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Gloria Kilawe, Marietha Maguta na Hamis Katandula. Walithibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na dawa hizo haramu. 

Upande wa utetezi, ukiongozwa na Mawakili Augustine Kusalika na Nehemia Nkoko, ulijaribu kupinga ushahidi kwa kudai kuwa mshtakiwa alikamatwa kabla ya tukio na kwamba kesi ilichochewa na chuki binafsi. Hata hivyo, hoja hizo zilitupiliwa mbali na Mahakama, ikiridhia ushahidi wa Jamhuri.

Akisoma hukumu, Jaji Kisanya alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umejitosheleza na kuthibitisha kosa bila kuacha shaka yoyote. 

Aidha, Mahakama imetoa maagizo ya kisheria kuhusu vielelezo ikiwemo kuteketezwa kwa  cocaine  iliyokamatwa, kurudisha baadhi ya mali binafsi za mshtakiwa, huku gari lililotumika kusafirisha dawa hizo na fedha taslimu TZS 4,100,000 zikichukuliwa hatua maalum za kisheria.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 (R.E. 2023), kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito unaozidi gramu 200  adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.Hivyo, hukumu hii ni onyo kali kwa jamii kwamba biashara ya dawa za kulevya haitavumiliwa nchini.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464