` DC KISHAPU AZINDUA CHANJO NA UTAMBUZI WA MIFUGO-MIFUGO 892,000 KUPATA CHANJO

DC KISHAPU AZINDUA CHANJO NA UTAMBUZI WA MIFUGO-MIFUGO 892,000 KUPATA CHANJO

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi akizungumza wakati akizindua chanjo na utambuzi wa mifugo Kata ya Mwamashele Wilayani humo Septemba 16,2025

Na Suma Salum – Kishapu

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amezindua rasmi kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo katika Wilaya hiyo, akisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wafugaji wananufaika na mifugo yao kwa kuongeza thamani, tija na kipato.


Akizungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika Kata ya Mwamashele, Septemba 16,2025 Mhe. Masindi akiwa ndiye Mgeni rasmi kwenye zoezi hilo amesema Serikali imeingia gharama kubwa kugharamia ruzuku ya 50% kwa chanjo zote, huku chanjo za kuku na vifaa vya utambuzi (heleni za kielektroniki) vikigawiwa bure.

“Serikali inataka kuona wafugaji wananufaika na mifugo yao kama mtaji halisi wa maendeleo. Wafugaji wakifuata kanuni za ufugaji bora ikiwemo kuchanja mifugo, kuwalisha vizuri na kuwanywesha maji ya kutosha, hakika faida itakuwa kubwa na umasikini utaondoka,” amesema Masindi.

Mhe. Masindi ameongeza kuwa zoezi Hilo litasaidia Utambuzi wa idadi halisi ya mifugo iliyopo nchini,Hupunguza wizi wa mifugo kwa sababu kila mnyama anatambulika kirahisi, Hurahisisha ufuatiliaji wa magonjwa na taarifa za mifugo, Kuongeza kipato cha wafugaji kwani Mifugo yenye afya huuzwa kwa bei nzuri sokoni na huchangia pato la kaya, Kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwani Mifugo yenye afya hutoa chakula bora kwa jamii na kuondoa udumavu na utapiamlo Kwa Watoto wadogo,wajawazito na wazee.


"Ndugu zangu sambamba na hayo zoezi litaisaidia serikali kupata uwezo wa kupanga maendeleo ya sekta ya mifugo Kupitia taarifa za utambuzi na kampeni za chanjo, serikali hupata takwimu sahihi kwa ajili ya sera, mipango na huduma bora za ugani.

Aidha amewataka wafugaji kuachana na dhana ya kujivunia idadi kubwa ya mifugo bila tija kwa familia.

“Urithi pekee usioharibika ni elimu. Wafugaji wahakikishe mifugo inaleta manufaa kwa familia, watoto wapate elimu bora, lishe bora izingatiwe na familia ijenge nyumba bora. Tuache kufuga kizamani bila faida,” ameongeza.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi akichoma Ng'ombe chanjo ya ugonjwa wa homa ya mapafu wakati akizindua rasmi kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo Kata ya Mwamashele Wilayani humo Septemba 16,2025Mkuu wa Idara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, Mwita Mwijarubi akizungumza kwenye uzinduzi wa chanjo na utambuzi wa mifugo Kata ya Mwamashele Wilayani humo Septemba 16,2025 ambapo mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilayani Kishapu,Mwita Mwijarubi Mwita, amesema katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, chanjo ya kuku imefanikiwa kutolewa kwa asilimia 100, huku zoezi zima la chanjo likiwafikia wafugaji kwa asilimia 87.

Mwijarubi amebainisha kuwa hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa tishio la magonjwa kwa mifugo, huku wafugaji wengi wakionesha mwamko wa kushiriki kikamilifu.

Awali, Mratibu wa Chanjo ya Mifugo Wilaya ya Kishapu, Bw. John Mchele, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya mapafu kwa ng’ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo, na ndui,kideri na mafua kwa kuku.

Mchele amefafanua kuwa Serikali imetoa ruzuku kubwa, ambapo Ng’ombe: Mfugaji atalipia Tsh. 500 badala ya 1,000,Mbuzi na Kondoo: Mfugaji atalipia Tsh. 300 badala ya 600,Kuku wa kienyeji: Dozi 300,000 zimetolewa bure.

Wamepokea Dozi ya Ng’ombe 450,000, Dozi ya Mbuzi na Kondoo 442,000 huku Dozi ya Kuku ikiwa 300,000 na Heleni za kielektroniki zikitolewa bure kwa ajili ya utambuzi wa mifugo.

“Mpango huu utasaidia kupata takwimu sahihi za mifugo, hivyo kurahisisha utoaji huduma na kupanga bajeti ya dawa na malisho,” amesisitiza Mchele.
Mratibu wa Chanjo ya Mifugo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, John Mchele akizungumza kwenye uzinduzi wa chanjo na utambuzi wa mifugo Kata ya Mwamashele Wilayani humo Septemba 16,2025 ambapo mgeni rasmi akiwa ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Mwamashele na Wafugaji wameonesha furaha yao kwa kampeni hiyo,Daudi Gamaya na Jilala Charles Maige na kusema chanjo ya sotoka kwa Mbuzi na Kondoo ilikuwa tishio kubwa kwa mifugo yao, lakini sasa wanaamini ugonjwa huo utadhibitiwa.

“Tunashukuru kwa chanjo na heleni tulizopewa, lakini bado tungeomba Serikali itusaidie pia dawa za minyoo kwa ruzuku angalau ya nusu gharama,” amesema Gamaya.

Nae Mwekezaji na mfugaji kutoka Kata ya Mwamashele, Khalidi Hamadi Hilal amepongeza jitihada za Serikali kwa kuwasaidia kupunguza gharama za chanjo na utambuzi wa mifugo.

“Kampeni hii ni faida kubwa kwa wafugaji. Tupo tayari kushirikiana kikamilifu ili kuongeza thamani ya mifugo yetu na kupata masoko ya uhakika,” amesema Hilal.

Kampeni hiyo inalenga kuhudumia wafugaji wote wa Wilaya ya Kishapu yenye jumla ya Kata 29 na Vijiji 117, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya mifugo na kuinua uchumi wa Wananchi.
Mwekezaji na mfugaji kutoka Kata ya Mwamashele Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Khalidi Hamadi HilalMfugaji kutoka Kata ya Mwamashele Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Daudi GamayaMfugaji kutoka Kata ya Mwamashele Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Jilala Charles Maige


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464