` RUWASA YAREJESHA HUDUMA YA MAJI NYASAMBA

RUWASA YAREJESHA HUDUMA YA MAJI NYASAMBA


Na Marco Maduhu, KISHAPU

WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kishapu, umetatua changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiwakabili wakazi wa Kijiji cha Nyasamba, baada ya pampu ya kisima kirefu kuharibika na kusababisha huduma hiyo kukosekana kwa zaidi ya siku mbili na sasa huduma imerejea.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana wananchi wa kijiji hicho,wamesema kutokana na kuharibika kwa pampu ya kisima, walilazika kutumia maji ya kwenye mabwawa ambayo siyo salama.
Mmoja wa wananchi hao Leah Samweli,amesema kutokana ukosefu wa huduma hiyo ya majisafi na salama, walipata shida kutumia maji ambayo siyo salama,lakini sasa wanaishukuru RUWASA kwa jitihada zao za matengenezo ya haraka na kurejesha huduma.

“Tunashukuru RUWASA kwa urejeshaji wa huduma ya maji hapa kijijini,ila ombi letu kwa serikali ituletee Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria, ili tuondokane kabisa na tatizo la ukosefu wa maji, sababu ya kuharibika kwa Pampu ya kisima,”amesema Leah.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyasamba Martin Kafumu,amesema kijiji hicho kina Kaya 800,na kuishukuru RUWASA kwa kurejesha huduma ya maji na kuokoa afya za wananchi.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu,Mhandisi Dickson Kamazima,amesema ukosefu wa maji kijijini humo,ulisababishwa na kuharibika kwa Pampu ya kisima kirefu kinachohudumia matangi ya Bubiki na Nyasamba.

Amesema, kwa sasa wamefunga Pampu mpya, na huduma za Majisafi na Salama zimerejea kama kawaida.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464