Serikali kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (PFSRT) inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo, imetoa mafunzo ya ugani kwa maafisa ugani 1,701 nchini kote. Lengo ni kuwafikia jumla ya maafisa ugani 4,000 ndani ya kipindi cha miaka mitano, ambao watawafikia wakulima zaidi ya milioni 1.5.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma, Mratibu wa Programu hiyo Bw. Timotheo Semguruka amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za ugani nchini.
“Mafunzo haya yamewawezesha maafisa ugani kutumia teknolojia mbalimbali za kisasa, ikiwemo mfumo wa M-Kilimo unaowezesha huduma za ugani kutolewa kwa njia ya TEHAMA. Hii itawawezesha wakulima wengi zaidi kufikiwa kwa wakati,” amesema Semguruka.
Ameongeza kuwa programu hiyo inalenga kubadilisha sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi, ushauri wa kitaalamu na teknolojia bora ili kuongeza uzalishaji na tija ya kilimo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464