` KISHINDO CHA KISIASA: AHMED ALLY SALUM AANZA MBIO ZA UBUNGE SOLWA

KISHINDO CHA KISIASA: AHMED ALLY SALUM AANZA MBIO ZA UBUNGE SOLWA

Sauti za hamasa, nyimbo za mshikamo na umati wa watu waliofurika leo katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ziliashiria tukio kubwa la kisiasa: Ahmed Ally Salum amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Solwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kiongozi huyu, aliyeidhinishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alipokelewa kwa kishindo kikubwa na mamia ya wanachama, viongozi na wapenzi wa chama waliomsindikiza kwa shangwe na nderemo, wakionesha mshikamano wa dhati na matumaini mapya kwa Solwa.

Baada ya kuchukua fomu, Ahmed Ally Salum amewashukuru wananchi na wanachama kwa mshikamo wao, huku akiahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika nyanja za afya, elimu, maji, kilimo, biashara na miundombinu.

“Nina imani kubwa kuwa mshikamano wetu ndiyo ngao ya ushindi. Tukiungana, Solwa itaendelea kusonga mbele kwa maendeleo endelevu,” amesema kwa kujiamini.

Wananchi waliokuwa sehemu ya tukio hilo wamesema uteuzi wake ni uthibitisho kwamba CCM imeweka mbele kiongozi sahihi, mwenye dira na rekodi ya utendaji uliowagusa wengi kwa matokeo chanya.

Kwa pamoja wameahidi kusimama naye bega kwa bega kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
 2025.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464