` KATAMBI ACHUKUA FOMU ZA UTEUZI, AAHIDI UMOJA NA USHINDI KWA CCM SHINYANGA MJINI

KATAMBI ACHUKUA FOMU ZA UTEUZI, AAHIDI UMOJA NA USHINDI KWA CCM SHINYANGA MJINI

 

Mgombea Ubunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Patrobas Katambi, amechukua Fomu za Uteuzi za kugombea nafasi ya Ubunge zilizotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Katambi amechukua fomu hizo leo Jumapili, Agosti 24, 2025, kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Ally Mohamed Liuye akiwa ameambatana na viongozi wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini pamoja na madiwani wateule wa chama hicho ikiwa ni ishara ya mshikamano na maandalizi ya ushindi wa kishindo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu za uteuzi, Mhe. Patrobas Katambi amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua hiyo na pia kuipongeza Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendesha mchakato wa uteuzi kwa uwazi na kumteua kugombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini. 

Ameeleza kuwa heshima hiyo kubwa imetolewa kwake si kwa sababu ya uwezo wake binafsi, bali kwa imani ya chama na wananchi waliompa nafasi hiyo, akimshukuru pia Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mgombea Mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo.

Katambi amewashukuru wananchi wa Shinyanga Mjini kwa heshima kubwa ya mara nyingine tena kumpa nafasi ya kuwatumikia, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa chombo cha kutimiza ndoto na maono yao bila kujali makundi wala tofauti za kifamilia, kisiasa au kijamii. 

Aidha, amewapongeza watia nia wenzake waliowania ubunge kwa tiketi ya CCM kwa mshikamano waliouonyesha kwa kumpa pongezi na kuahidi kushirikiana naye kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo.

Katika ujumbe wake, Katambi amesisitiza mshikamano akisema: “Sifurahii Shinyanga Mjini yenye makundi, ninawaomba kwa unyenyekevu tuwe wamoja katika kila hatua ya safari hii ya uchaguzi. Ikiwa kwenye mchakato huu tumekwaruzana au kukoseana kwa namna yoyote, naomba msamaha na mimi pia nimesamehe kwa moyo wa dhati. Sasa tuwe timu moja tukipigania ushindi wa chama chetu.”

Ameongeza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao unategemea mshikamano wa wana-CCM na wananchi kwa ujumla, akihimiza tahadhari dhidi ya aina yoyote ya usaliti, akisema chama hicho kikiwa imara na wamoja hakina shaka ya kushinda kwa kishindo kikuu. 

Katambi amewataka wana-Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio lijalo la kuchukua fomu rasmi za uteuzi kwenye Tume ya Uchaguzi, akisisitiza kuwa hilo ni tukio muhimu kwenye safari ya ushindi wa CCM.


Aidha Katambi amewaomba wananchi kumuombea kwa Mungu katika jukumu alilokabidhiwa, akisisitiza kuwa ushindi atakaoupata si wake binafsi bali wa wananchi wote wa Shinyanga Mjini na CCM kwa ujumla, na kuhitimisha kwa maneno yake ya kawaida: “Ninawapenda sana, tukutane site, na mapenzi ya Mungu yakatimie.”

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464