
Na Sumai Salum-Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi amewaasa wahitimu wa mafunzo ya jeshi la akiba Wilayani humo kuutunza ujuzi waliopata,kudumisha amani na kutetea maslahi ya Taifa.Mhe.Masindi ametoa wito huo Agosti 26,2025 katika hafla ya kufunga mafunzo ya jeshi la akiba yaliyofanyika katika uwanja wa Jengoni Negezi Kata ya Ukenyenge na kusema kuwa serikali ina matumaini makubwa kuwa wahitumi hao watakuwa mfano wa kuigwa katika jamii na kuwa chachu ya mabadiliko.
"Vijana wangu leo hii tunashuhudia mkihitimu mafunzo haya ya jeshi la akiba, leo ni siku yenu muhimu inayoingia katika kitabu cha historia ya maisha yenu" amesema Masindi.
"Nimeambiwa awali wakati mnaanza mafunzo haya mnamo tarehe 30,4,2025 mlikuwa 46, lakini kwa bahati mbaya wengine wakaishia njiani na sasa mnahitimu mkiwa jumla yenu 37 bila shaka hii ni faraja kubwa kwetu, sasa na nyinyi hakikisheni mnazingatia miiko na maadili mliyofundishwa na wakufunzi wenu itawasaidia kuaminika na kufanikiwa sana" ameongeza Mkuu huyo wa WilayaMkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga ambae pia ni mgeni rasmi wa hafla ya kilele cha mafunzo ya jeshi la akiba Mhe.Peter Masindi (kushoto) akipitishwa kukagua gwalide la wahitimu 37 na Mkufunzi na Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilayani humo Meja. Linus Elias (kulia) Agosti 26,2025 katika viwanja vya Jengoni Kata ya Ukenyenge
Pia ametumia jukwaa hilo kuwahakikishia wahitimu kuwa, serikali inatambua changamoto ya ajira inayowakabili na kusema kuwa tayari Uongozi wa Wilaya unafanya jitihada za kuwasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za serikali zenye mahitaji ya vijana wenye sifa za mafunzo ya aina hiyo ili watoe kipaumbele katika ajira pindi zitakapojitokeza.
Kwa upande wake mshauri wa Jeshi la akiba Wilayani humo Meja.Linus Elias amezipongeza jitihada za ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika kwa namna moja ama nyingine huku akisema wamefanikiwa kuwajengea uzalendo,nidhamu,kushiriki shughuli za kiuchumi,utu na ulinzi kulisaidia Jeshi la Kujenga Taifa JKT,Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ pindi watakapohitajika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bw.Emmanuel Johnson amewapongeza wahitimu hao kwa uvumilivu na kuwataka kujiunga kwenye vikundi ili wapate mkopo wa 10% na kujikwamua kiuchumi.
"Kuhusu suala la Kombati ninaahidi kugharamikia kombati zao pamoja na kuwapa kipaumbele kwenye suala la ulinzi kwenye ofisi zetu za umma" Amesema Johnson.
Jumla ya wahitimu 37 wametunukiwa vyeti vya kozi ya mafunzo ya Jeshi la akiba yaliyoanza mwezi Aprili 30,2025 wote wakiwa wavulana.
Sambamba na hayo Mkuu wa Wilaya amefanya na kuhitimisha ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Tarafa ya Negezi katika Kijiji cha Ukeyenge,Mwaweja na Mwamadulu huku akiwataka watendaji kuhakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo na wananchi kuunga juhudi za maendele zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Masindi ataendelea na ziara yake katika Tarafa ya Mondo Kesho Kijiji cha Nyasamba,Mwajiningu na Itongoitale.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi

Katibu Tawala Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Bi.Fatma H. Mohammed

Mshauri wa jeshi la akiba Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Meja.Linus Elias

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson





























Mnunuzi wa pamba kampuni ya Alliance wakipakia pamba baada ya kununua kutoka kwa wananchi wa Mwamadulu kupitia Amcos ya Mwamadulu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga

Muonekano wa baadhi ya bidhaa zilizoko gulio la Mwamadulu kila Jumanne lililoko Kata ya Lagana Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga




