Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,ameendelea na ziara yake ya Kata kwa Kata katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi,huku akitoa maagizo kwa watalaamu na viongozi wa Taasisi za serikali,kuwa kero hizo zitatuliwe na wampatie mrejesho.
ziara hiyo imefanyika leo Agosti 26,2025 katika Kata za Lyamidati, Lyabukande na Mwakitolyo Kijiji cha Nyaligongo, akiwa ameambatana na Watalaamu wa Halmashauri,na viongozi kutoka Taasisi za Serikali kujibu kero za wananchi.
Akizungumza mara baada ya kusikiliza kero za wananchi,amewaagiza Wataalamu na viongozi wa Taasisi za serikali,kuzishughulikia kero zote ambazo zimewasilishwa na wananchi, na kisha kumpatia mrejesho wa utatuzi wake.
"Kero zote ambazo zimewasilishwa na wananchi naagiza zitatuliwe na nipatiwe mrejesho juu ya utatuzi wake, na hii kero ta tatizo la umeme kuwa mdogo hapa kijiji cha Kizungu, naiagiza TANESCO,hadi kufikia Ijumaa,nipate mpango wenu kwa barua lini mtaleta "Transformer" hapa kijijini,"amesema Mtatiro.
"Pia ameagiza kwa ndugu ambao wanataka kumdhulumu mali mwezao ambaye ana ulemavu, na wamekuwa wakiitwa na serikali wanagoma, naagiza wakamatwe na waletwe ofisini kwangu," ameongeza Mtatiro.
Amewataka pia wananchi, kuendelea kuchangia shughuli za maendeleo, ikiwamo kuanzisha ujenzi wa maboma na kisha serikali kumalizia na kuanza kutoa huduma.
Akizungumza na wananchi wa Lyabukande, amewataka wanapokuwa wakiona mtu yotote ambaye wanamtilia mashaka kijijini hapo,kwamba watoe taarifa ili apate kukamatwa na siyo kukubali kutapeliwa kama ilivyotokea kwa baadhi ya wananchi kutapeliwa nguzo za umeme na vishoka.
Mtatiro akiwa Kijiji cha Nyaligongo,ameagiza Ofisi ya Madini,wawasilishe taarifa ya vikundi vyote 15 vya Wachimbaji Wadogo wa dhahabu kwa kuwashilikiana na Mwanasheria wa Halmashauri,na kwamba kila "file" waeleze malalamiko yote ya kila kikundi,ili aone namna ya kutatua matatizo yao.
Ameeleza pia kusikitishwa na miradi ya maendeleo kushindwa kukamilika kwenye maeneo hayo ya Machimbo ikiwamo Zahanati, na kuagiza Makampuni ambayo yameingia mikataba kumalizia miradi hiyo ya maendeleo na kushindwa kutekeleza, kwamba wampatia "details" za kutosha ili azibane kumalizia jenzi hizo.
"Hatuwezi kuwa na Madini na kuonekana kama laana,bali madini yawe baraka kwetu, nina agiza wiki ijayo niandaliwe kikao kingine hapa Nyaligongo tuje tuzungumza changamoto za madini tu hapa kuna issue kubwa," amesema Mtatiro.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mwita Waryuba,amesema kwamba kero zote ambazo zimewasilisha, baadhi zimesha anza kutatuliwa ikiwamo kutengewa bajeti na nyingine zitaendelea kutatuliwa.
Akizungumzia suala upungufu wa Watumishi katika Zahanati ya Kizungu, amesema tatizo hilo la upungufu wa Watumishi ni la nchi nzima,lakini wataangalia kuongeza Watumishi.
Katika mikutano hiyo, wananchi waliwasilisha kero mbalimbali,zikiwamo za ubovu wa barabara,ukosefu wa maji,umeme,upungufu wa Watumishi sekta ya Afya na Elimu, pamoja na kukosekana kwa mawasiliano sababu ya kutokuwapo mitandao ya simu.
Kero zingine ni Zahanati ya Kijiji cha Nyaligongo kutofanya kazi licha ya kukamilika,baadhi ya Wachimbaji wadogo wa dhahabu kutopewa mikataba na wamiliki wa maduara,pamoja na kudai Makampuni ya Wachina kuwanyanyasa wachimbaji, na umeme kukatika mara kwa mara maeneo ya Migodi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mwita Waryuba akitoa majibu ya kero za wananchi