Siasa za Shinyanga Mjini zimepata msisimko mpya baada ya Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, jina lake kurejea tena kwenye orodha ya walioteuliwa kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa wapenda siasa, hii ni habari inayotafsiriwa kama mapambano ya siasa za kizazi kipya dhidi ya changamoto za miji mikubwa.
Katambi, kijana machachari na mwanasiasa mwenye mvuto, anarejea akibeba jeuri ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na heshima ya kuwa kiongozi wa serikali ya awamu ya sita.
Katika kipindi cha ubunge wake, Katambi amekuwa sauti ya vijana na ajira, akitumia nafasi yake bungeni na serikalini kushinikiza mageuzi ya ajira, uwezeshaji wa vijana na maboresho ya mazingira ya kazi.
Ndiyo maana kwa wapiga kura wa Shinyanga Mjini, jina lake halikuwashangaza , bali limechochea ari ya hamasa mpya.
Kwa mtazamo wa wachambuzi, Katambi anabeba sura mbili za kisiasa: mwanasiasa wa kitaifa anayesimamia ajenda kubwa za vijana, lakini pia mtu wa mtaani anayeguswa na changamoto za wananchi wa kawaida.
Huo mchanganyiko ndio unaotajwa kumweka kwenye nafasi ya kipekee katika kinyang’anyiro cha mwaka huu.
Lakini je, Shinyanga Mjini – mji uliozoea upinzani mkali kisiasa utakuwa tayari kumpa ridhaa ya pili Katambi? Je, nguvu yake ya kisiasa itaendelea kuwa dira ya ushindi wa kishindo kwa CCM?
Kwa sasa ni wazi kuwa kurudi kwa jina la Katambi kwenye ulingo wa siasa za Shinyanga Mjini kunafungua ukurasa mpya wa mjadala: Ni Mgombea gani wa Chama cha Upinzani ataweza kumtikisa kijana huyu anayebeba alama ya siasa za kizazi kipya?
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464