` AZZA HILLAL HAMAD KUPEPERUSHA BENDERA YA CCM 2025

AZZA HILLAL HAMAD KUPEPERUSHA BENDERA YA CCM 2025

 


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua Azza Hilal Hamad kugombea ubunge wa Jimbo jipya la Itwangi mkoani Shinyanga, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. 

Jimbo la Itwangi limeundwa baada ya mgawanyo wa Jimbo la Solwa Mkoani Shinyanga, hatua inayolenga kuongeza uwakilishi na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa eneo hilo. Kwa mara ya kwanza, wakazi wa Itwangi watapata mbunge wao maalum kupitia sanduku la kura.

Azza Hilal Hamad si mgeni katika siasa za Shinyanga. Amehudumu kama Mbunge wa Viti Maalum kwa kipindi cha miaka 10, akijijengea heshima kama kiongozi mahiri na mwenye msimamo thabiti katika kutetea masuala ya wanawake, vijana na maendeleo ya jamii.

Katika kipindi cha utumishi wake bungeni, Azza amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha miradi ya kielimu, afya na uwezeshaji kiuchumi, jambo lililomfanya kujijengea taswira ya kiongozi anayeguswa na changamoto za wananchi wake. 

Wanajamii wa Itwangi wanamuelezea kama “kiongozi wa watu,” mwenye ukaribu na mshikamanisho wa kijamii.

Kwa uteuzi huu, Azza anakuwa mwanasiasa wa kwanza kupewa nafasi ya kuwania ubunge katika Jimbo la Itwangi kupitia CCM , hatua inayoonesha imani kubwa ya chama kwake na matarajio makubwa ya wananchi wanaosubiri kujipatia mwakilishi wao bungeni.

Kwa Azza, uzoefu wake bungeni na mchango wake katika jamii unampa mtaji wa kisiasa unaoweza kumsaidia kushinda kwa kishindo katika kinyang’anyiro cha kwanza kabisa cha jimbo jipya la Itwangi.

Kwa sasa macho na masikio ya wanasiasa na wananchi mkoani Shinyanga yameelekezwa Itwangi, wakisubiri kuona namna Azza Hilal Hamad atakavyoibeba bendera ya CCM kuelekea ushindi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464