Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) leo tarehe 23 Agosti 2025 imetangaza majina ya wagombea wa nafasi za ubunge watakaokwenda kuipeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Miongoni mwa waliopata baraka za NEC ni Ahmed Ally Salum, ambaye ameteuliwa rasmi kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Solwa, mkoani Shinyanga.
Uteuzi huu unamrejesha Ahmed Ally Salum katika kinyang’anyiro cha kisiasa akiwa na uzoefu wa muda mrefu katika shughuli za maendeleo ya wananchi na mchango mkubwa ndani ya CCM.
Kupitia uteuzi huu, chama kimeonesha imani kubwa kwake na kumkabidhi jukumu la kuendelea kuwatumikia wananchi wa Solwa.
Wananchi wa Jimbo la Solwa wamepokea kwa shangwe taarifa hizi, wakieleza matumaini yao kuwa uteuzi wa Ahmed Ally Salum ni mwanzo wa hatua mpya ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.
Uteuzi huu ni sehemu ya maamuzi makubwa yaliyofanywa na kikao cha NEC cha CCM kilichoketi Dodoma, ambapo majina ya wagombea wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Visiwani yametangazwa.
Hatua inayofuata ni maandalizi ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, ambapo CCM imedhamiria kushinda kwa kishindo.