Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Paschal Katambi, ameteuliwa rasmi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.
Uteuzi huo ulifanyika jana kupitia kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Ally Mohamed.
Akizungumza mara baada ya kuteuliwa, Katambi ametuma salamu kwa vyama vya upinzani, akibainisha kuwa kampeni zake zitakuwa za kistaarabu, zikitawaliwa na hoja na kueleza utekelezaji wa miradi aliyofanikisha katika kipindi chake cha miaka mitano, sambamba na ahadi za awamu inayofuata.
Amesema yeye hata kuwa Mbunge wa Propaganda na kupiga porojo, bali ni mtu wa vitendo kwa kuhakikisha wananchi wa Shinyanga wanapata maendeleo na kuinuka kiuchumi kupitia fursa za mikopo mbalimbali ambayo inatolewa na serikali.
“Nashukuru kuteuliwa na INEC kugombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama changu cha CCM,nawaomba wananchi wa Shinyanga wanichague tena niendelee kuwa Mbunge wao, na kazi yangu wameiona kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kila mwenye macho amejionea mwenyewe kasi kubwa ya maendeleo, mimi nitaendelea kuwa Mbunge wa Vitendo,”amesema Katambi.
“Nawaomba pia wawachague Madiwani wote wanaotokana na CCM, pamoja na kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,ili CCM ishinde kwa kishindo na kuendelea kuwatumikia katika kuwaletea maendeleo,”ameongeza Katambi.
Aidha,amesema mambo mengi ya kimaendeleo ameyafanya kwa wnaanchi wa Jimbo la Shinyanga katika sekta mbalimbali ikiwamo kuboresha huduma za Afya kwa kujenga Zahanati,Vituo vya Afya,kukarabati Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na Rufaa ya Mkoa.
Amesema amejenga miundombinu ya barabara, madaraja,makaravati, masoko,ujenzi wa shule mpya 10,Msingi Tano na Sekondari Tano,amejenga Zahanati 8,ujenzi wa Machinjio ya kisasa,upanuzi Uwanja wa Ndege,na sasa wanajenga Stendi mpya ya kisasa ya Mabasi,na Barabara ya kiwango cha Lami kutoka kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Amesema pia amechochea upatikanaji wa vyuo vya kati vitatu (3)na Chuo Kikuu kimoja.
"nimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwaunganisha Chama na Serikali,Chama na wanachama, Chama na wananchi,pia nimefanya maendeleo ya Chama ikiwamo ujenzi wa ofisi mbili za Chama za kisasa ya Ibadakuli na Chibe zenye zaidi ya sh.milioni 104 kwa kipindi cha miaka yangu mitano ya Ubunge,"amesema Katambi.
Amesema, mambo mengi atayazungumza atakapoanza kampeni zake, kwa kuelezea nini ambacho amekifanya kwa kila Kata.
Hata hivyo, CCM leo Agosti 28 inazindua rasmi kampeni zake za kitaifa kwa ajili ya kunadi sera na kuomba kura za madiwani, wabunge na rais katika Uchaguzi Mkuu huo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464