` KATAMBI MOSHI MWEUPE UBUNGE AIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI SHINYANGA MJINI

KATAMBI MOSHI MWEUPE UBUNGE AIBUKA KIDEDEA KURA ZA MAONI SHINYANGA MJINI


Katambi Moshi Mweupe Ubunge aibuka kidedea kura za maoni Shinyanga Mjini

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini aliyemaliza muda wake, Patrobas Katambi, ameibuka kidedea katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata kura 2,922 kati ya kura 3,930 zilizopigwa.

Kura halali zilikuwa 3,898 huku kura 32 zikiharibika.

Waliokuwa wakichuana na Katambi katika kinyang’anyiro hicho ni Stephen Masele aliyepata kura 874, Paul Brand kura 34, Aboubakar Mukadamu na Hassan Fatihu kila mmoja kura 25, Hosea Karume kura 16, na Eustard Ngatale aliyepata kura 10.

Akizungumza baada ya kutangaza matokeo hayo, leo Agosti 4,2025 Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Hamisa Chacha, alisema matokeo hayo ni ya awali na kwamba vikao vya chama bado vinaendelea ili kumpata mgombea rasmi atakayekiwakilisha chama hicho katika Uchaguzi Mkuu.

“Tunawaomba wagombea wote wawe watulivu kusubiri maamuzi ya vikao vya chama,” alisema Chacha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anord Makombe, amesema uchaguzi huo umefanyika kwa uwazi na kuzingatia misingi ya demokrasia.

“Napenda kuwapongeza wagombea wote, hata wale ambao kura zao hazikutosha lakini wamekubali matokeo na kusaini, hiyo ndiyo demokrasia,” amesema Makombe.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464