MAKAMBI KANISA LA WASABATO MTAA WA SHINYANGA MJINI 2025 YAHITIMISHWA,WAOMBEA UCHAGUZI MKUU UFANYIKE KWA AMANI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
WAUMINI la Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa wa Shinyanga Mjini wamehitimisha sikukuu ya vibanda (Makambi)ambayo yamefanyika kwa muda wa siku 7,huku wakiombea Uchaguzi Mkuu 2025 ufanyike kwa Amani na utulivu.
Makambi hayo yalianza Agosti 16, 2025 na yamehimishwa leo Agost 23,yakiwa na ujumbe usemao “Nitakwenda nikimtumaini Yesu”.
Mnenaji Mkuu katika Makambi hayo ni Mchungaji Isaya Iligo kutoka Jimbo la North West Tanzania Field ya Bukoba, ambapo katika Mahubiri yake,pamoja na mambo mengine ameombea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ufanyike kwa amani na utulivu.
Amesema Taifa la Tanzania ni kisiwa cha amani na kielelezo cha umoja na mshikamano,na kuwasihi Watanzania kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 waufanye kwa amani na utulivu.
Mchungaji Iligo,Amesema amani ndiyo kila kitu, na ndiyo maana shughuli za kiroho zinafanyika na watu wana muabudu Mungu na kueleza kwamba kuna baadhi ya nchi haziwezi kukusanyika na kuabudu pamoja,na kusisitiza amani ya Tanzania inapaswa kudumishwa.
“huwezi kuthamini amani kama hujapitia uzoefu wa vita, amani ni Tunu ya thamani katika Taifa letu, tusikubali ivurugwe katika uchaguzi wa mwaka huu,bali tuilinde na kuombea uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu,”amesema Mchungaji Iligo.
Aidha, katika mahubiri yake amesisitiza pia kama mtu hana uhakika na jambo unalotaka kuzungumza, au jambo hilo kama litaleta ugomvi katika jamii ni vyema akanyamaza kimya.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa wa Shinyanga Mjini Gadiel Mziray,amesema Makambi hayo ni kuwakusanya waumini wote katika kukuza maadili yao kwa ajili ya kumtegemea mwenyezi Mungu katika maisha yao.
Amesema, Makambi hayo yamekuwa na neno kuu linalosema “Nitakwenda Nikimtumaini Yesu”ambao linejengwa katika Zaburi 62:8 ikiagiza kwamba enyi watu mtumaini Mungu siku zote, ifunueni mioyo yenu mbele zake,Mungu ndiyo kimbilio letu,na kwamba fungu hilo linatoa mwaliko kwa waumini kutegemeza matumaini yao kwa mwenyezi Mungu.
“Siku 7 zote katika Makambi haya waumini wamekuwa wakija na kushinda hapa Kanisani kujifunza neno la Mungu, tuna amini baada ya mkutano huu,wanakwenda kuwa raia wema katika Taifa letu na katika Jamii zetu,sababu wanayo maadili na watii wa sheria,”amesema Mchungaji Mziray.
Naye,Mzee kiongozi wa Kanisa la Wasabato Shinyanga Mjini Dk.Elison Maeja, ameelezea maana ya Makambi, kwamba katika Biblia yanaitwa Sikukuu ya Vibanda, na neno la Mungu kupitia Kitabu cha Mambo ya Walawi 23:35-36,Mungu ameagiza kila mwaka watoto wake wakutane pamoja kumfanyie sherehe,na Mkutano wa kukutana na Mungu wao, kwa mafundisho mbalimbali.
Naye Moja wa Waumini wa Kanisa hilo Happyness Soppy, amesema Makambi hayo yamewajenga kiimani, sababu wamejifunza mambo mbalimbali ya neno la Mungu.
Aidha, kila Mwaka Kanisa la Waadventista Wasabato nchi nzima, hufanya sherehe hiyo ya sikukuu ya vibanda (Makambi).
TAZAMA PICHA👇👇
Mchungaji Isaya Iligo kutoka Jimbo la North West Tanzania Field ya Bukoba Kanisa la Wasabato akihubiri katika Makambi ya Wasabato Mtaa wa Shinyanga Mjini.
Mchungaji wa Kanisa la Wasabato Mtaa wa Shinyanga Mjini Gadiel Mziray akizungumza katika Makambi hayo.
Makambi ya Kanisa la Wasabato Mtaa wa Shinyanga Mjini Ibada ikiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464












































