ZAIDI YA WANANCHI 500 WAPATIWA HUDUMA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA KUTOKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE KATIKA HOSPITALI YA RUFAA MKOA SHINYANGA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MGANGA Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John, amesema zaidi ya wananchi 500 wa Mkoa wa Shinyanga, wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya Kibingwa ya Magonjwa ya Moyo, kupitia Kambi Maalumu ya Madkatari Bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwete JKCI.
Kambi ya Madaktari hao ilianza kutoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, kuanzia Agosti 18 na kuhitimishwa leo Agosti 22,2025.
Dk.Luzila akizungumza leo na waandishi wa habari,amesema lengo la Kambi hiyo ilikuwa ni kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya Moyo kwa wananchi,pamoja na kuongeza ujuzi wa wataalamu,na kushukuru wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.
“lengo kwa siku moja ilikuwa ni wastani wa kuona wananchi 100 kwa siku, lakini tulikuwa tukipata zaidi, na ndani ya siku hizi tano, wananchi zaidi ya 500 wamepatiwa huduma za matibabu ya kibingwa ya Magonjwa ya Moyo,”amesema Dk. Luzila.
Dk.John Luzila.
“Pia Madaktari hawa, wamewajengea uwezo Wataalamu wetu wa Afya 15, kutoka Hospitali yetu ya Rufaa na Hospitali za wilaya za Halmashauri zetu,”ameongeza.
Aidha,amesema licha ya Kambi hiyo ya Madaktari Bingwa kutamatika,anatoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo, kwamba waendelee kuhudhuria Kliniki ya Magonjwa ya Moyo kwenye Hospitali hiyo pamoja na kufanya uchanguzi, ambayo hutolewa mara mbili kwa kila wiki siku ya Jumanne na Ijumaa.
Dk.Mlagwa Yango.
Katika hatua nyingine, amesema hospitali hiyo hutoa huduma zingine za kibingwa zikiwamo za Afya ya Mama na Uzazi, Magonjwa ya ndani,upasuaji wa mifupa,upasuaji wa jumla na huduma za kibingwa za macho.
Naye Dakatri Bingwa wa Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)Dk. Mlagwa Yango, amesema wakati wa utoaji wa huduma hizo, magonjwa mengi ambayo yalibainika ni Shinikizo la Juu la damu, Moyo kutofanya kazi vizuri, na kwamba watu 50 wamewapatia Rufaa ya kwenda kwenye Taasisi hiyo kupatiwa matibabu zaidi.
Ametoa wito pia kwa wananchi,kwamba ili kuepukana na Magonjwa hayo ya Moyo, waepuke kula Chumvi nyingi, vyakula vya wanga,Sukari, na kuwashauri pia wafanye mazoezi ya mara kwa mara.
Nao baadhi ya wananchi ambao wamepata huduma hiyo, wameipongeza serikali kwa kuwaletea madaktari hao bingwa na kuomba kambi hiyo iwe inafanyika mara kwa mara.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



