` SERIKALI KUZIHUDUMIA CHAKULA NA MALAZI FAMILIA ZINAZOSUBIRI NDUGU ZAO 18 KUOKOLEWA AJALI YA MGODI

SERIKALI KUZIHUDUMIA CHAKULA NA MALAZI FAMILIA ZINAZOSUBIRI NDUGU ZAO 18 KUOKOLEWA AJALI YA MGODI

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

SERIKALI mkoani Shinyanga imeanza kutoa huduma za chakula na malazi kwa familia 18 ambazo ndugu zao bado wamefukiwa kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo katika machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amebainisha hayo leo Agosti 18, 2025 alipofika katika eneo la ajali kukagua maendeleo ya zoezi la uokoaji na kuzungumza na familia zinazolisubiria ndugu zao kuokolewa.

Mboni ameaema kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto zinazowakabili familia hizo wakati wakisubiri ndugu zao kuokolewa.

“Hapa tuna familia za watu 18 ambao bado ndugu zao hawajaokolewa,lakini familia zingine zina watu wengi sana waliokusanyika hapa,sisi kama serikali tumeona ni vyema wakateue wawakilishi wachache, hata watu wawili kutoka kila familia, ambao watabaki hapa mgodini, ili tupate kuwahudumia kwa malazi na chakula,” amesema Mboni.

Ameongeza kuwa kuwa na watu wengi kwenye eneo la tukio bila huduma za msingi za kibinadamu ni hatari, hivyo serikali imeona umuhimu wa kuweka utaratibu huo.

Aidha, amesema kuwa zoezi la uokoaji linaendelea vizuri, na kwamba njia za kupitisha hewa tayari zimetengenezwa ili kufanikisha jitihada za kuwafikia wachimbaji 18 waliobaki chini ya mgodi.

Ameaema tangu ajali hiyo kutokea Agosti 11 Mwaka huu na kuwafukia watu 25, tayari watu saba wametolewa, kati yao watatu wakiwa hai na wanne wamefariki dunia. Miili ya marehemu hao imeshakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafamilia wameishukuru serikali kwa kuwapatia huduma za chakula na hifadhi, huku wakiiomba iongeze kasi ya uokoaji ili ndugu zao waweze kuokolewa mapema.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464