` KAMBI MAALUM YA MADAKTARI BINGWA MAGONJWA YA MOYO KUTOKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE WATIA KAMBI SHINYANGA

KAMBI MAALUM YA MADAKTARI BINGWA MAGONJWA YA MOYO KUTOKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE WATIA KAMBI SHINYANGA

Kambi Maalum ya Madaktari Bingwa Magonjwa ya Moyo ‘JKCI’ yatia kambi Shinyanga

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

KAMBI Maalum ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewasili mkoani Shinyanga kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani.
RC Mboni Mhita.

Madaktari hao wamewasili leo Agosti 18, 2025 na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ambapo wanapiga kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa siku tano mfululizo.

Mboni,amepongeza ujio wa madaktari hao akibainisha kuwa hatua hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi kupata huduma za kibingwa karibu, bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi kufanya uchunguzi na kupata matibabu ya magonjwa ya moyo,huduma hizi ni muhimu kwa afya zetu," amsema Mboni.

Aidha, Mboni ameishukuru pia Hospitali ya Aga Khan kwa kuendesha kambi ya kutoa huduma za saratani ya mlango wa kizazi katika hospitali hiyo,huku akisisitiza umuhimu wa na kutoa elimu ya chanjo kwa wasichana ili kuimarisha kinga dhidi ya saratani hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge, amesema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za moyo kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya nchini.

“Mbali na huduma za matibabu, pia tutatoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakisababisha mshtuko wa moyo,"amesema Dk.Kisenge.
Amesema pia wanapendeza kianzishwe kitengo maalum cha moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na kwamba wao wapo tayari kutoa mafunzo na msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa ufanisi mkoani humo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, amesema kambi hiyo ya madaktari bingwa itakuwa hospitalini hapo kuanzia Agosti 18 hadi 22, na wananchi wanakaribishwa kujitokeza mapema ili kupata huduma hizo.

Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kuhudumiwa,wameeleza kufurahishwa na ujio wa madaktari hao, wakisema kuwa ni fursa adimu inayowaondolea gharama kubwa za kusafiri kufuata huduma nje ya mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita(kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dk.Peter Kisenge.
Wananchi wa Shinyanga wakiendelea na huduma katika Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464