Mmoja wa majeruhi ajali mgodini afariki akipatiwa matibabu, Naibu Waziri wa Madini Kiruswa atoa maelekezo kwa sekta ya madini
Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro ametangaza kufariki kwa mmoja wa mafundi waliookolewa wakiwa hai katika ajali ya mgodi wa kikundi wachapakazi uliopo katika kijiji cha Mwongozo kata ya Mwenge Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 ambapo maduara haya yalititia baada ya kuwa yakifanyiwa ukarabati, ndipo ardhi ilipotitia na kufunika watu 25 ambapo kati yao watatu waliokolewa Agosti 12, 2025 na mmoja leo Agosti 13 lakini amefariki wakati akifanyiwa matibabu.
Akizungumza na wananchi leo Agosti 13, 2025 wakati akimkaribisha Naibu waziri wa madini Steven Kiruswa amesema madaktari walifanya juhudi za kuokoa maisha yake lakini hawakufanyikiwa kwani alikuwa na hali mbaya sana,
“Jana tulifanikiwa kuokoa watu watatu na mtu wa nne tumemuokoa leo asubuhi akiwa hai ambaye ni Emmanuel Kija (zaidi ya 20) lakini alikuwa na hali mbaya hadi wakamuunganishia hewa ya ziada (Oxygen) lakini juhudi hazikuzaa matunda na mida ya jioni akapoteza maisha, lakini pia mmoja anayeitwa Fulano Peter amepewa rufaa ya kwenda Bugando, Mwanza” amesema Mtatiro.
Aidha, kutokana na ajali hiyo Naibu Waziri wa madini Steven Kiruswa ametoa maelekezo kwa watu wa madini ikiwa ni pamoja na kutoruhusu watu kufanya ukarabati maeneo tofautitofauti,
“Natoa maelekezo kwa watu ya madini kama ni ukarabati ufanyike kwenye duara moja baada ya jingine maana watu wanapoingia sehemu tofautitofauti wakifanya ukarabati ndio inachangia mitikisiko kuzidi na kusababisha udongo kuporomoka, pia ni vyema kutoa ushauri wa kitaalamu katika kufanya marekebisho bila kuhatarisha maisha ya watu pia nawaomba tuwe na subira na kumuomba Mungu ili wenzetu tuwaokoe wakiwa hai” amesema Kiruswa.