` TANESCO YATOA ELIMU YA KUPIKIA KWA UMEME, KULINDA MIUNDOMBINU

TANESCO YATOA ELIMU YA KUPIKIA KWA UMEME, KULINDA MIUNDOMBINU


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga limetumia fursa ya tamasha la utamaduni wa Kisukuma, Sukuma Festival, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo, sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kupata huduma bora za umeme.

Kupitia banda lao la maonesho katika tamasha hilo, TANESCO imetoa elimu kwa wananchi kuhusu njia rahisi za kufanya maombi ya umeme kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa Nikonekt, unaorahisisha mchakato wa kuunganishiwa umeme kwa haraka na uwazi zaidi.

Aidha, wananchi wamepata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia majumbani, ikiwemo umeme na gesi safi, kwa lengo la kuboresha afya za watumiaji, kupunguza gharama za matumizi ya nishati, na kulinda mazingira dhidi ya ukataji miti ovyo.

Vilevile, TANESCO imeelimisha umma juu ya usalama na ulinzi wa miundombinu ya umeme, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa endapo kutatokea wizi, uharibifu au hitilafu yoyote ya miundombinu.

Katika kuimarisha huduma kwa wateja, wananchi wamehamasishwa kutumia huduma ya bure ya simu kwa kupiga 180 kupitia mpango wa Nihudumie, unaowawezesha kuripoti matatizo, dharura au kutoa maoni kuhusu huduma za umeme bila gharama yoyote.

TANESCO imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kusogeza huduma bora, salama na za kisasa karibu na wananchi, kwa kutumia mifumo ya kidijitali na kutoa elimu endelevu kwa jamii, ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika masuala ya nishati.







Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464