RC Mboni Ahitimisha Ziara Kahama na Vipaumbele Sita kwa Maendeleo ya Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo amehitimisha ziara yake kikazi aliyoifanya kwa halmashauri zote Sita za mkoa huo katika Manispaa ya Kahama na kutumia nafasi hiyo kuwasisitizia watumishi wa halmashauri hiyo juu ya vipaumbele sita muhimu ambavyo serikali ya mkoa inavitaka vizingatiwe kwa maendeleo ya wananchi.
Akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo, RC Mhita alieleza kuwa kwa sasa Shinyanga ipo katika hatua ya kusukuma maendeleo kwa kasi, hivyo ni lazima kila mtumishi afanye kazi kwa uadilifu na uzalendo.
"Watumishi mnatakiwa kujikita katika uwajibikaji wa kweli, kufuata sheria na miongozo iliyowekwa, na kuhakikisha kila mmoja wenu anatimiza wajibu wake kwa maslahi ya wananchi wetu," alisema Mboni.
Alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni:
1. *Uwajibikaji wa kila mtumishi*,
2. *Uadilifu kazini*,
3. *Kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria na miongozo ya serikali*,
4. *Kusikiliza na kutatua kero za wananchi*,
5. *Kuepuka matumizi mabaya ya mapato ya ndani*,
6. *Kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza vyanzo vipya vya mapato*.
Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza kuwa mkoa wa Shinyanga hauwezi kusonga mbele kama watumishi hawatakuwa na maono ya pamoja ya kubeba dhamana ya maendeleo ya wananchi.
Aliwataka watumishi hao kushirikiana na uongozi wa wilaya kuhakikisha kuwa kila senti ya mapato ya ndani inatumika kwa ufanisi na miradi ya maendeleo inaleta tija kwa jamii.
Mhe. Mhita pia alieleza kuwa mkoa utaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maagizo hayo na kwamba hatua zitachukuliwa kwa watakaobainika kuvuruga mwelekeo wa maendeleo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464