Taasisi ya Flaviana Matata imekabidhi mradi wa WASH Shule ya Sekondari ya Salawe wilayani Shinyanga
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
TAASISI ya Flaviana Matata imekabidhi rasmi mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya maji, afya na usafi wa mazingira (WASH), katika Shule ya Sekondari Salawe mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wanafunzi hasa wa kike kusoma katika mazingira salama na rafiki.
Uzinduzi na makabidhiano ya mradi huo umefanyika leo Julai 23,2025 ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro,ujenzi ambao umetekelezwa na Taasisi ya Flaviana Matata kupitia ufadhili wa Shirika la kimataifa
Diamonds Do Good.
Mradi huo umehusisha ujenzi wa matundu 12 ya vyoo vya kisasa, sehemu ya kunawia mikono, chumba maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu, chumba cha wasichana kujisitiri wakati wa hedhi, pamoja na sehemu ya kuchomea taka, hususan taulo za kike zilizotumika.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtariro akizungumza kwenye hafla hiyo, amesema mradi huo ni hatua muhimu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu, hasa kwa kuhakikisha watoto wa kike wanakuwa na mazingira bora ya kujifunzia.
“Nawapongeza sana Taasisi ya Flaviana Matata kwa moyo wao wa kizalendo. Mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za afya na mahudhurio duni ya wanafunzi hasa wa kike shuleni kutokana na kuwapo na chumba maalum cha kujistiri hedhi” amesema Mtatiro.
Kwa upande wake Meneja Miradi Taasisi ya Flaviana Matata,Lineth Masala, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za taasisi yake za muda mrefu kusaidia watoto wa kike kutimiza ndoto zao kupitia elimu.
“Tunaamini kuwa mazingira salama, yenye usafi na staha, ni haki ya kila mtoto. Kupitia miradi ya aina hii, tunajitahidi kuondoa vikwazo vinavyowarudisha nyuma wasichana, hasa wakati wa hedhi,” amesema Masala.
Nao baadhi ya wanafunzi shuleni hapo akiwamo Maryciana Juma,wameishukuru taasisi hiyo kwa kuwajengea mradi huo, hasa chumba maalumu cha kujistiri hedhi ambacho kitawasaidia kutunza utu wao.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka shuleni hapo, zaidi ya wanafunzi 665 watanufaika moja kwa moja na mradi huo, hali ambayo inatarajiwa kuongeza mahudhurio, kuboresha afya na hata kiwango cha ufaulu.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akikata utepe.