RC Mboni Kuongoza Mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mkoani Shinyanga
Na RS SHINYANGA.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni M. Mhita, anatarajiwa kuongoza mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaowasili rasmi mkoani Shinyanga tarehe 3 Agosti 2025, ukitokea mkoani Tabora. Mwenge huo utapokelewa katika Kituo cha Mabasi cha Kagongwa, kilichopo Wilaya ya Kahama.
Katika ziara hiyo ya Mwenge, unatarajiwa kukimbizwa kwa umbali wa kilometa 819.2 ndani ya halmashauri zote sita za mkoa huo, ukipitia miradi 44 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 17.3.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Mwenge huo utakagua, kufungua na kuzindua miradi ya afya, elimu, maji, miundombinu na shughuli za vijana na wanawake zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mhita, amewaomba wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge huo wa kitaifa kama ishara ya mshikamano, uzalendo na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha huduma kwa jamii.
“Mapokezi haya ni ya kihistoria, hivyo ni fursa kwa wananchi kuonyesha mshikamano wao na kufuatilia kwa ukaribu ujumbe wa Mwenge wa Uhuru unaohamasisha amani, maendeleo, mapambano dhidi ya rushwa na matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Mboni.
Mwenge wa Uhuru 2025 unatarajiwa kuwa chachu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa miradi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi Mkuu.
Kauli Mbiu ya Mwenye wa Uhuru mwaka huu inasema"Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa amani na utulivu”