` RC MBONI AKABIDHI PIKIPIKI,LAPTOP,SIMU NA DIRA ZA MAJI KWA CBWSOs ZA RUWASA SHINYANGA

RC MBONI AKABIDHI PIKIPIKI,LAPTOP,SIMU NA DIRA ZA MAJI KWA CBWSOs ZA RUWASA SHINYANGA

RC MBONI AKABIDHI PIKIPIKI,LAPTOP,SIMU NA DIRA ZA MAJI KWA CBWSOs ZA RUWASA SHINYANGA

Na Marco Madsuhu,SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amekabidhi pikipiki sita, kompyuta mpakato (laptop), simu janja na dira za maji kwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSOs), vilivyo chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani humo.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Julai 29, 2025, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Mboni akizungumza mara baada ya kumaliza kukabidhi vitendea kazi hiyo, amewataka watoa huduma hao CBWSOs, Kwamba wavitunze na vitumike kwa madhumuni kusudiwa, ya kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi, na kutekeleza adhima ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo kichwani Mwanamke.
“Nawapongeza RUWASA kwa kazi nzuri ambayo mmekuwa mkiifanya kwa kukahikikisha wananchi wa Shinyanga wanapata huduma ya maji safi na salama na kumtua ndoo kichwani mwanamke, na leo hii mmewanunulia CBWSOs vitendea kazi, ambavyo vitawasaidia kuwafikia wananchi na kuwapatia huduma,”amesema Mboni.

Pia,ametoa wito kwa Watumishi wa RUWASA kwamba waendelee kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, na kila mmoja awajibike katika eneo lake, ili kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa Maji vijijini ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2025.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela,awali akisoma taarifa,amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia fedha za mapato ya ndani ya CBWSOs, wamenunua vitendea kazi kwa ajili ya kuwarahisishia utendaji kazi watoa huduma hao ya maji ngazi ya jamii.

Ametaja vitendea kazi hivyo, kuwa ni Pikipiki 12 , na kwamba Kati ya hizo, leo ndiyo wamekabidhi Pikipiki Sita na kusalia zingine 6 ambazo zinaendelea na utaratibu wa manunuzi kupitia GPSA, wamenunua pia Dira 100 za Maji aina ya Bylan,ili kupunguza upotevu wa maji.
Aidha,amesema pia Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA wamewanunulia CBWSOs Laptop Tatu,Simu za Smart Phone 20, kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji wa takwimu kwa vyombo 20 kwa Mkoa wa Shinyanga.

“Vitendea kazi vyote hivi, thamani yake ni Sh.Milioni 71.510,000,”amesema Mhandisi Julieth.
Katika hatua nyingine,ametaja mafanikio ambayo yamepatikana baada ya CBWSOs kuunganishwa na Mfumo wa Malipo ya Kielekitroniki (GePG),kwamba wameongeza ufanisi wa makusanyo ya fedha zitokanazo na maduhuli ya maji.

Anasema katika mwaka wa fedha 2024/2025, CBWSOs zote 28 za Mkoa huo zimekusanya jumla ya sh.Bilioni 2.4, ikilinganishwa na Mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo kilikusanya kiasi cha sh.Bilioni 1.6.

Mmoja wa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya Jamii (CBWSOs) Valeria Jonasani,akizungumza kwa niaba ya wenzake,amesema vitendea kazi hivyo watavitunza na kuvitumia ipasavyo, ili kutoa huduma bora ya majisafi na salama kwa wananchi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita (kulia)akikata Utepe kukabidhi Pikipiki Sita kwa CBWSOs, (kushoto)ni Meneja wa RUWASA wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akikabidhi Dira ya Maji.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akikabidhi Laptop.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akikabidhi Simu.
Muonekano wa Pikipiki.
Picha ya pamoja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464