
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa kwa njia ya kidijitali ambapo ameongea na Wajumbe wa Mkutano huo nchi nzima kwa njia ya mtandao tarehe 26 Julai, 2025 katika ukumbi wa mkutano wa NEC (White House) Makao Makuu ya CCM, Jijini Dodoma.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 Blog
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kimeandika historia mpya kwa kupitisha kwa kishindo marekebisho ya Katiba yake ya mwaka 1977 (Toleo la Mei 2025), hatua inayoonesha wazi ukuaji wa misingi ya demokrasia ndani ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CCM uliofanyika Jumamosi Julai 26,2025 kwa njia ya mtandao, wajumbe 1,915 kati ya 1,931 wameshiriki upigaji kura ya maoni.
Kati ya hao, kura 1,912 ziliunga mkono marekebisho, tatu zikiharibika na hakuna kura ya kupinga, hali iliyopelekea uungwaji mkono wa asilimia 99.8. Matokeo hayo yametangazwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Haji Ussi Gavu.
Marekebisho hayo, yaliyoelezwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa ni madogo lakini ya kimkakati, yamelenga kutoa unyumbufu zaidi kwa Kamati Kuu ya CCM kuongeza idadi ya wagombea wanaoshiriki kura za maoni katika nafasi za ubunge, udiwani na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Marekebisho hayo ni pamoja na: Kufanyia mabadiliko Ibara ya 105(7F) ya Katiba ya CCM kwa kuruhusu Kamati Kuu kuongeza majina ya wagombea wa ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kulingana na uhitaji na Kurekebisha Ibara ya 91(6C) kwa mtiririko huo huo kwa upande wa nafasi za udiwani.
Kwa sasa, idadi ya majina ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani itaanzia watatu na kuendelea, badala ya ukomo wa majina matatu wa awali. Rais Dkt. Samia amesema hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa demokrasia ndani ya chama na kutoa nafasi kwa wanachama wengi zaidi kushiriki mchakato wa uongozi.
“Tulifanya maamuzi ya kupanua demokrasia katika kuchagua viongozi wa ngazi zote, jambo lililovutia wana-CCM wengi kuomba nafasi za uongozi. Hivyo, kubaki na wagombea watatu pekee haionekani kuwa busara tena,” amesema Dkt. Samia.
Amebainisha kuwa baadhi ya majimbo yalikuwa na hadi wagombea 39 au 40 waliokuwa wamejitokeza kuwania ubunge, hivyo Katiba ya zamani ilikuwa kikwazo kwa Kamati Kuu kufanya maamuzi sahihi.
“Kesho tunaanza kazi ya kuchuja majina, tutajitahidi kuingiza vijana wengi zaidi,” amesisitiza Rais Samia, akionyesha dhamira ya chama kuendelea kuwajumuisha vijana katika nafasi za uongozi kwa lengo la kuimarisha kizazi kipya cha viongozi ndani ya CCM.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewapongeza wajumbe kwa ushiriki mkubwa, akisisitiza kuwa mchakato wa upande wa udiwani utaendelea kama kawaida kwa kuwa tayari umesharuka hatua iliyofanyiwa marekebisho.
