Mwenyeki waTume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC Jaji Jacobs Mwambegele.
INEC YAONYA WATENDAJI WA UCHAGUZI KUWA VYANZO VYA MALALAMIKO KWA VYAMA VYA SIASA UCHAGUZI MKUU 2025
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),imewataka watendaji wa Uchaguzi Mkuu 2025, wajiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi.
Hayo yamebainishwa leo Julai 21,2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)Jaji Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mafunzo kwa Watendaji wa Uchaguzi kutoka Mikoa ya Simiyu na Shinyanga,Mkutano utakaofanyika kwa muda wa siku tatu mkoani Shinyanga kuanzia leo Julai 21-23.
Amesema Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)inatoa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi Mkuu, katika kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo,na kwamba wajiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi, bali wazingatie katiba,sheria,kanuni na miongozo kutoka Tume.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu ,mnao katika uendeshaji wa uchaguzi hakikisheni mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea, ikizingatiwa kwamba baadhi ya mambo yamekuwa yakibadilika hasa sheria za uchaguzi, na msije kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa,”amesema Jaji Mwambegele.
Amewataka pia kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura ili kuviwezesha kupanga mawakala,na wakati wa kuwaapisha mawakala watoe taarifa mapema kwa vyama hivyo,pamoja na kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kuziba mapungufu pamoja na kuweka mpangilio mzuri ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.
“Dhamana mliyopewa ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani ni kubwa na nyeti na nimuhimu kwa mustakabili wa Taifa letu,hivyo Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi inawategemea katika utendaji wenu na mtekeleze majukumu yenu kwa weledi mkubwa,”amesema Jaji Mwambegele.
Naye Jaji Mkazi Mfawidhi wa Mahakama wilaya ya Shinyanga Goodselda Kalumuna, kabla ya kuwaapisha watendaji wao wa uchaguzi,amewataka wasimamie viapo vyao vya kutunza siri na kujitoa kutokuwa wanachama wa Chama chochote cha siasa katika kipindi chote cha Uchaguzi Mkuu.