` USAJILI NI WA LAZIMA VITUO VYA KULEA WATOTO SI HIARI - DAVID LYAMONG

USAJILI NI WA LAZIMA VITUO VYA KULEA WATOTO SI HIARI - DAVID LYAMONG

USAJILI NI WA LAZIMA VITUO VYA KULEA WATOTO SI HIARI - DAVID LYAMONG

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyan ga, Bw. David Lyamong, ametoa wito kwa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto na wazee kuhakikisha wanakamilisha usajili wa vituo vyao mara moja ili kuimarisha usalama na ustawi wa makundi hayo nyeti katika jamii.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa huduma za kijamii, amesema baadhi ya vituo vinaendelea kutoa huduma bila kusajiliwa, jambo linaloweza kuhatarisha maisha ya watoto na wazee kwa kukosa uangalizi wa kitaalamu na wa kisheria.

"Usajili si wa hiari bali ni hitaji la kisheria linalolenga kulinda haki, usalama na utu wa watoto na wazee wanaolelewa kwenye vituo hivi," amesema Bw. Lyamong, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuweka viwango vinavyokubalika kisheria na kijamii.
Bw. Lyamong amesisitiza kuwa mkoa umejipanga kutoa usaidizi wa karibu kupitia wataalamu wa ustawi wa jamii waliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha taratibu zote za usajili zinafuatwa kwa ufanisi na wepesi.

Aidha, amewatahadharisha wale wanaoendesha vituo bila kufuata sheria kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kufunga vituo visivyo na usajili.
Huduma nzuri ni ile inayotolewa kwa mujibu wa taratibu, ikiwemo usajili rasmi ili kuhakikisha usalama wa watoto na wazee, kuepuka vishoka, na kurahisisha usimamizi wa serikali. Hivyo, ni lazima kusajili vituo vyao rasmi ili kuepuka mkanganyiko na hatari zisizo za lazima.

Katika hatua nyingine, Bw. Lyamong amebainisha kuwa kuna utofauti mkubwa kati ya vituo vya kulelea watoto mchana (Day Care Centres) na shule. Ameeleza kuwa Day Care ni vituo vya huduma ya malezi kwa watoto wadogo kwa kipindi kifupi cha mchana, tofauti na shule ambazo zimesajiliwa kutoa elimu rasmi. Hivyo, ni muhimu kwa wamiliki kutambua tofauti hiyo na kusajili huduma zao kwa mujibu wa aina ya huduma wanazotoa.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Tawala huyo, usajili si wa hiari bali ni hitaji la kisheria linalolenga kulinda haki, usalama na utu wa watoto na wazee wanaolelewa kwenye vituo hivyo. Amesisitiza kuwa mkoa wa Shinyanga una dhamira ya kuhakikisha kila kituo kinatoa huduma bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika kisheria.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464